TGNP YATOA SOMO LA MALEZI BORA NA YANAYOFAA KWA WATOTO KWA WANA-DGSS

WAZAZI na walezi wametakiwa kuwa na aina au mfumo wa malezi ya Kidemokrasia ikiwemo kujenga mahusiano mazuri pamoja na kutilia maanani hisia za mtoto au watoto.

Wito huo umetolewa leo Julai 3, 2024 katika Semina za Jinsia na Maendeleo ambazo hufanyika kila Jumatano katika Viwanja vya TGNP- Mtandao Mabibo Jijini Dar es Salaam.

Mwanasaikolojia Sylvia Sostenes wakati akiwasilisha mada kuhusu malezi, amewasihi walezi wote kuwa na muda wa kutosha wa kukaa na watoto wao kama nyenzo ya kufuatilia mwenendo wa mtoto au watoto.

Mwanasaikolojia huyo ameendelea kwa kufafanua kuwa, kulea ni pamoja na kuwekeza katika mahitaji muhimu kama lishe bora, afya ya mwili, roho na akili, elimu, ulinzi, muda kwa ajili ya kuchangamana na watoto.

Katika uwanda wa kisaikolojia, Bi. Sylvia ameeleza kuwa, malezi ni mchakato uliosheheni vitu vingi ndani yake lakini kubwa zaidi ikiwemo na kumpatia mtoto mahitaji yake na huduma muhimu.

"Malezi ni mchakato wa maandalizi ya mtoto utakaomwezesha mtoto kukua, kukubalika, kujikubali, kushiriki katika shughuli za kijamii na kiutamaduni kwa kumlinda, kumjumuisha na kumpatia mahitaji na huduma za msingi" alisema Bi. Sylvia na kuongeza kuwa

"Iwapo malezi ni mchakato wa maandalizi ya mtoto basi sharti iwepo mikakati toka kwa wazazi/walezi ili kufanikisha hili. Kwasasa tunaishi kwenye huu mtindo huria ambao ni wa kujipatia Watoto na kuwaacha wakue. Watoto wanajilea wao wenyewe."

Akichangia katika semina hiyo, Joseph Bulemo amesema kwa sasa, familia nyingi hazina ukaribu na watoto jambo linalopelekea matukio ya ukatili kwa watoto kuendelea kutokea.

Bw. Bulemo pia ameyataja malezi ya kimabavu dhidi ya watoto kama sababu inayopelekea watoto kuwa karibu na wazazi au walezi.

Naye Nantaika Maufi ameshauri wazazi kuwa karibu na watoto katika kila hatua kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kugundua mapema mabadiliko yoyote au pindi watoto wapatapo changamoto yoyote au kufanyiwa ukatili huku akipinga hoja ya ugumu wa maisha na shughuli za utafutaji kama kikwazo cha kutokuwa karibu.

Kwa upande wake Mpegwa Noah amewataka wazazi na walezi kuwa na umoja wa dhati na uchungu sawa kwenye malezi kwa watoto wao, watoto wa majirani na watoto wengine wowote kwa kufanya hivyo itachangia watoto katika maadili mazuri kwa kuoata malezi bora.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post