Balozi wa Brazil nchini Tanzania Mheshimiwa Gustavo Martins Nogueira amesema uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Brazil na Tanzania ni wa muda mrefu na mashirikiano kati ya nchi hizi mbili yanaendelea kuimarika kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa hapa nchini.
Mheshimiwa Balozi Nogueira amesema haya leo jijini Dar es Salaam alipokutana na kuzungumza na Dkt. Felix Wandwe ndc, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim. Viongozi hawa, pamoja na mambo mengine wamejadili fursa zilizopo za ushirikiano wa kitaaluma baina ya Tanzania na Brazil.
“Kutokana na ushirikiano mzuri uliopo wa Kidiplomasia baina ya Brazil na Tanzania, Brazil ina ajenda ya maendeleo nchini Tanzania na imekuwa ikishirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za kilimo, nishati, madini na elimu. Kwa upande wa Zanzibar kumekuwa na ushirikiano katika sekta ya afya hasa afya ya uzazi” amesema Mheshimiwa Balozi Nogueira.
Akizungumza kuhusu kilichokuwa Chuo cha Diplomasia kupewa jina la Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Balozi Nogueira ameipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kumpa heshima mwanadiplomasia nguli Dkt. Salim Ahmed Salim. Hatua hii ya kukipa Kituo jina hilo amesema kuwa ni kutambua na kuthamini mchango mkubwa alioutoa kwa Taifa na nchi yake, Afrika na sehemu nyingine duniani.
Hatua hii amesema kuwa ni kama ambavyo nchi ya Brazil ilifanya kwa Taasisi ya Diplomasia ya Rio Branco ya kuipa Taasisi hiyo jina la mwanadiplomasia mahili Rio Branco.
“Tunatambua kazi na shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Kituo hiki, nampongeza Mheshimiwa January Makamba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Uongozi wa Wizara kwa kukisemea na kukitangaza Kituo hiki cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ndani na nje ya nchi. ” amesema Mheshimiwa Balozi Nogueira.
Mheshimiwa Balozi Gustavo Martins Nogueira amesema anafahamu hivi karibuni kuna Kongamano la Kiswahili linatarajia kufanyika nchini Cuba ambalo litawakutanisha wadau mbalimbali wa Kiswahili. Kongamano hili linaonyesha ni jinsi gani lugha ya Kiswahili ni ya kipekee na inazidi kukua duniani. Amesema kwa upande wao watafuatilia kuona namna gani lugha ya Kiswahili inaweza kufundishwa nchini Brazil.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kituo, Dkt. Felix Wandwe ndc amemshukuru Mheshimiwa Balozi Nogueira kwa kukitembelea Kituo na kupata muda wa kujadili fursa mbalimbali zilizopo za mashirikiano ya Kitaaluma kati ya Brazil na Tanzania.
Amesema, ujio wa Mheshimiwa Balozi Nogueira kwetu ni mwanzo wa hatua kupitia Wizara yetu ya kuwepo kwa mazungumzo ya mashirikiano baina ya Taasisi ya Diplomasia ya nchini Brazil na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim. Kituo, pamoja na majukumu mengine kina wajibu pia wa kukuza mashirikiano na mahusiano na mataifa mbalimbali kwa lengo la kujenga heshima na taswira nzuri ya nchi.