Na Mwandishi Wetu.
Ripoti mpya ya Baraza la Utalii Duniani (Travel & Tourism Council,WTTC) iitwayo “ Travel and Tourism: Economic Impact Research 2024,” iliyotolewa Juni 26, 2024 jijini London, UK, inaonesha Tanzania kuwa moja ya Mataifa ambayo yameendelea kunufaika kiuchumi na mageuzi makubwa yanayoendelea nchini chini ya Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya utalii kama ifuatavyo:
Kwa ujumla inasema ripoti hiyo, utalii na safari viliingizia Tanzania TZS Trilioni 18.6 mwaka jana 2023, ikiwa ni rekodi kubwa ya mapato kuwahi kutokea ikizidi ile ya mwaka 2019 (kabla ya uviko) kwa nyongeza ya asilimia 4;
Kiasi kilichotumiwa na watalii kwa huduma mbalimbali (visitor spending levels) kimepanda mwaka jana 2023 na kuweka rekodi ya juu zaidi ambapo watalii wa nje walitumia TZS trilioni 8 huku wa ndani wakitumia TZS trilioni 3.7 sawa na ongezeko la asilimia 11.1 na 12.8 mtawalia ikilinganishwa na mwaka 2019.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa ajira katika sekta ya utalii Tanzania mwaka 2023 zilifikia watu milioni 1.4 ikiwa ni ongezeko la ajira 97,000 lakini zikiwa pungufu kidogo kwa asilimia 7.4 ikilinganishwa na rekodi ya juu mwaka 2019.
Kwa mwaka 2024 matarajio ya mchango wa sekta ya utalii nchini, inasema taarifa hiyo ya WTTC, ni kufikia TZS Trilioni 20.4 na kukua hadi TZS Trilioni 31 katika miaka kumi ijayo (kiwango ambacho ni takribani robo tatu ya Bajeti ya sasa ya Serikali ya Trilioni 49) huku ajira zikitarajiwa kuweka rekodi mpya na ya juu zaidi kuwahi kutokea nchini kwa mwaka huu kufikia zaidi ya ajira milioni 1.5.
“Sekta ya Utalii ya Tanzania inazidi kuimarika kila uchao ikiweka rekodi za juu kuwahi kufikiwa,” anasema Mtendaji Mkuu wa WTTC Julia Simpson kuhusu ripoti ya Tanzania.
Aidha, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika ambazo mafanikio yake yamechambuliwa kwa kina katika Tovuti ya Baraza hilo. Soma hapa: https://wttc.org/news-article/tanzanias-travel-and-tourism-reached-record-breaking-levels-in-2023