Na Mariam Kagenda _Kagera
Wadau mbalimbali halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera wamekutana pamoja kujadili jinsi ya kuongeza bidii katika suala la kupambana na changamoto ya udumavu na utapiamlo kwa wananchi.
Wadau hao kutoka maeneo tofauti tofauti wamekutana Julai 4, 2024 katika kikao kazi cha lishe kikilenga zaidi taathimini ya utekelezaji wa mradi walishe uliokuwa ukitekelezwa na Shirika la PANITA kilichofanyika Manispaa ya Bukoba ambapo katika majadiliano hayo suala la elimu ya lishe limebainika kuwa bado ni changamoto inayowakabili wananchi walio wengi.
Wamefafanua kuwa kutokana na jamii kuwa na uelewa mdogo juu ya ulaji wa vyakula mchanganyiko na vyenye virutubishi imepelekea baadhi ya wananchi kutokukubali kubadilika nakuendelea kutumia vyakula kwa mazoea ambapo wametoa mfano jamii inavyokula chakula aina ya ndizi kwa wingi bila ya mchangayiko wa chakula kingine.
Joseph matope ni kaimu afisa elimu awali na msingi wilaya amesema kuwa Bukoba na Kagera kwa ujumla vyakula vipo vya kutosha lakini matumizi yamekuwa ni hafifu mno.
"Vyakula wanavyo magimbi yapo, maharage yapo, mboga za majani zipo, mihogo na vingine vingi vipo lakini hawavichanganyi wakati wa ulaji, watoto wanawapa ndizi pekee kuanzia asubuhi, mchana na kuendelea, tubadilike wote ili kuyafikia malengo, amesema afisa Joseph Matope"
Afisa huyo pia ameeleza kuwa sekta ya elimu jitihada zimefanyika nakuhakikisha shule nyingi halmashauri hiyo zinatoa huduma ya uji na chakula kwa wanafunzi japo shule zinazotumia unga uliorutubishwa ni chache kutokana na mashine zinazosindika unga wa lishe kuwa chache maeneo ya Bukoba.
Jambo jingine lililoelezwa kuchochea udumavu nipamoja na baadhi ya wazazi kutokuwa tayari kupokea maelekezo muhimu kutoka kwa watalaamu wa afya juu ya utekelezaji wa lishe, maelezo ambayo yametolewa naye mwalimu Paschal Ngaiza.
"Tunapolisimamia suala hili la lishe tujitowe ufahamu wazazi hawa wengine ni wakorofi wamekuwa wagumu hata kuchangia chakula cha watoto shuleni, hii lishe imekuwa pasua kichwa kwa hiyo tunatakiwa wote kujikakamua na kujipanga vilivyo kuibadilisha jamii yetu hii" mwalimu Paskal akisisitiza.
Hata hivyo kwa upande wao PANITA ambao ni mwavuli wa mashirika ya kijamii yanayoshughulika na masuala ya afya na lishe kwa kushirikiana na Gain pamoja na Sanku wanaotekeleza mradi wa urutubishaji chakula shuleni .
Kupitia Afisa mradi Lubango Charles wamezitaja shughuli za miradi ya lishe zilizoteketezwa kwa Bukoba DC ikiwemo ya kukutana na viongozi wa halmashauri na wadau wa lishe, kukutana na viongozi wa kata hasa kata ya Kemondo, kuhamasisha uanzishwaji wa bustani za mbogamboga shuleni, wamezifikia shule tano.
Nyingine ni kuwajengea uwezo watalaamu wa afya ngazi ya jamii, kuelimisha jamii matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa, usimamizi shirikishi katika utekelezaji wa maazimio ya mradi na nyinginezo.
Akihitimisha taarifa Afisa Lubango amesema mradi huo kwa sasa umefika kikomo, hivyo ametoa wito akiwasihi wadau wote kupitia nyadhifa zao kujimudu na kuibeba kwa dhati dhana nzima ya lishe kwa kuifuatilia jamii ili kuona kama yanayoelimishwa yanatekezwa kwa ufanisi.
Kaimu afisa lishe wilaya Donald Kalenzo amebainisha na kusema kuwa lishe bora ni jambo ambalo limekuwa likipambaniwa zaidi katika halmashauri ya Bukoba ili kuhakikisha udumavu na utapiamlo unapungua kwa kiwango kikubwa na jamii ibakie kuwa salama kama yalivyo makusudi ya serikali.
Amewahimiza wadau wote kuungana pamoja kuupiga vita udumavu ili kuwalinda watu wote nakuwa na jamii yenye lishe bora kuanzia wanawake wajawazito na watoto.
Joanitha Jovin ni afisa lishe mkoa akipongeza juhudi za PANITA kwa kazi kubwa waliyoifanya Kagera amewakumbusha wadau kuwa udumavu ni adui ambaye anapaswa kutokomezwa ili kuinua afya ya jamii kwani Kagera ni mkoa wenye neema ya vyakula hivyo haina sababu ya kuwa katika hali ya udumavu kama ilivyo kwa sasa.
Licha ya pongezi na shukrani ametoa ombi kwa shirika hilo kurejea tena Kagera kwa miradi mingine ya lishe ili kuzifikia wilaya zote za mkoa kwani awamu hii ilizihusisha halmashauri tatu za Bukoba DC, Manispaa ya Bukoba na Muleba.
Social Plugin