Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFANYABIASHARA WAMLILIA RAIS SAMIA KUWAJENGEA MABANDA YA BIASHARA




Na Christina Cosmas, Morogoro

WAFANYABIASHARA wadogo wa soko la Mazimbu road Manispaa ya Morogoro wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwatazama kwa jicho la huruma na kuwajengea mabanda ya biashara ya kudumu kama ilivyo eneo la Feri -Mvomero na Mtumbatu -Gairo ili kuhudumia jamii na wasafiri wa nchi jirani wanaopita kwenye eneo hilo bila kuathiriwa na hoja ya kuondolewa pembezoni mwa barabara kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro- Dodoma.

Mwenyekiti wa soko hilo lenye wafanyabiashara zaidi ya 150 waliokaa kwa zaidi ya miaka 15 mahali hapo Khaji Hassan alisema hawapingi kuondoka kwenye eneo hilo kwa ajili ya kupisha upanuzi wa barabara sababu wanafahamu sheria haiwaruhusu kubaki hapo bali wamestushwa na tangazo la ghafla lililotolewa Julai mosi mwaka huu likiwataka kuwa wameshaondoka hadi ifikapo Julai 7 ambapo wao wakiwa hawajui mahali kwa kwenda kuendeleza biashara zao.

Hassan alisema wakiwa wafanyabiashara wa mali mbichi ikiwemo nyanya, embe, mananasi, machungwa, ndizi za kuiva, samaki na vingine wanashindwa kuondoka kutokana na kutopata mahali sahihi na Rafiki kwa kuuza biashara zao.

Alisema mara baada ya tangazo hilo walilazimika kuandamana kwa amani hadi ofisi ya Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Morogoro ili kujiridhisha ukweli wa tangazo hilo ambapo TANROADS waliwahakikishia kuwa kweli wanapaswa kuhama kwa mujibu sheria ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo na kulinda usalama wao.

Alisema wakalazimika kwenda kwa Mkuu wa Wilaya Morogoro Rebecca Nsemwa ambaye nae aliwahimiza kuhama kwa madai kuwa tayari wameshapewa maeneo ambayo hata wao hawayajui kwa sababu hawajaoneshwa maeneo yoyote ya kwenda mpaka sasa. 

Alisema wamekaa hapo muda mrefu wakiwa wanashabihiana kibiashara huku wakikopeshana, wengine wakiwa na mikopo kutoka taasisi za kifedha waliyolazimika kukopa mara baada ya kukumbwa na mafuriko ya msimu wa mvua uliopita ambapo wafanyabiashara wa hapo walikuwa waathirika wakubwa kwa kupoteza nyumba na vitu vya ndani.

 “nadhani Mheshmiwa DC tulivyomfuata alipozungumzia eneo analodai tumeoneshwa amemaanisha lile ambalo lilinunuliwa na wachache waliotaka kufanya biashara na baadae wakataka kuligeuza kuwa soko na wao ndio sababu ya kutufanyia figisu sisi ili twende pale ambapo sio Rafiki kwetu sababu gharama ni nyingi, tulipe vikazi, tulipe ushuru wa manispaa, kwa mitaji gani!, na sehemu yenyewe hakuna maji wala choo, tutaenda kufanyaje biashara zetu za matunda ambazo zinataka maji” alihoji mwenyekiti huyo.   

Wakizungumza kwa vilio na masikitiko wafanyabiashara hao akiwemo Getruda Kamnge aliiomba Serikali iwafikirie sababu eneo walilopo ni la kati wanawauzia wapita njia wakiwemo watu wanaoenda nchi za nje kama vile Burundi, Uganda na Zimbabwe na kwamba kuhamia mitaani hakutawasaidia kupata wateja kama hao wa barabarani.

Alisema wafanyabiashara walio wengi hapo Mazimbu road walikubwa na mafuriko na kukabiliwa na changamoto ya kubomoka kwa nyumba zao na vyombo kwenda na maji ambapo biashara hizo zinawasaidia kuanza kurejesha vitu vyao ambapo serikali iangalie namna ya kuhakikisha wanaejea eneo walilozoea kufanya biashara hata baada ya upanuzi wa barabara hiyo.

Naye Nicola Ngatunga ambaye anawatoto watatu yatima anaowalea aliiomba Serikali kuwapa muda wa kuhama hata miezi mitatu ili waweze kujipanga kuwa wanaenda wapi na wasiharibu biashara zao na kuwaondoa haraka kutawafanya kushindwa kurejesha hata mikopo waliyokopa ASA, OYA na kwingine kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Naye Maria Mwangi alimuomba Rais Samia kuwasaidia kuondokana na changamoto hiyo sababu wao kama wamama wanalea familia huku wengine wakiwa hawana wanaume na wengine ni wajane ambao wamelazimika kuingia mikopo ili wafanye biashara na kulea familia zao.

“sisi tunamlilia nani, wakubwa mtuangalie sisi ni wadogo, Maisha ni magumu sasa hivi, hatuwezi kudanga, umalaya hatuuwezi, kodi za nyuma zinatuumiza vichwa mama, tunakuja kwenye biashara saa mbili asubuhi na tunarudi nyumbani saa tano hata Watoto zetu wanasoma kwa shida, tupo chini ya miguu yako mama Samia tusikilize” alisema Mwangi.

Akizungumzia sakata hilo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Rebecca Nsemwa ametoa nyongeza ya siku saba kwa wafanyabiashara hao kuanzia tarehe 8 hadi 14 mwezi huu ili waondoke katika eneo hilo ili kupisha upanuzi wa barabara kwa mujibu wa sheria.

Nsemwa alisema wafanyabiashara hao hawana budi kuondoka kwenye maeneo hayo kwa kuwa tayari wameshaoneshwa maeneo ya kwenda kuendeleza biashara zao kupisha upanuzi wa barabarahiyo kwa kilometa tano kutoka msamvu hadi kwa chambo kata ha kihonda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com