Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKOPAJI WATAKIWA KUWA TAYARI KUANZA BIASHARA KABLA YA KUKOPA

Meneja masoko na uhamasishaji wa Taasisi ya kiserikali ya utoaji Mikopo ya Self Microfinance Fund (Self MF) kutoka makao makuu Linda Mshana

Na Christina Cosmas,  Morogoro 

WAKOPAJI nchini wanapaswa kujenga dhana ya kuwa tayari kuanza biashara kabla ya kukopa na kuacha kuchukua mikopo na kuiingiza kwenye sherehe na mambo ya anasa na kushindwa kurejesha kwa wakati. 

Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya ukopeshaji kwa asasi 55 za mikopo meneja Mikopo kutoka Taasisi ya Flonag Microfinance iliyopo Manyuki Grace Luena   alisema kufuatia elimu hiyo wanayopewa Self Microfinance mkoani hapa anaamini itasaidia kuondoa changamoto hiyo.

Luena alisema wakopaji hasa wanawake wamejenga tabia ya kutokopa kwa malengo na kuziingiza fedha zao kwenye masuala ya sherehe, kununua nguo au gari ambavyo haviingizi fedha yoyote na baadae kushindwa kurejesha kwa wakati na kusababisha taasisi kuyumba kimitaji.

Naye Mwenyekiti wa umoja wa wakopeshaji fedha mkoani Morogoro Raphael Wambura aliiomba serikali kuzitazama taasisi za kifedha zinazotoa huduma bila kibali na kuleta changamoto zinazoleta majina yasiyofaa ikiwemo kaushadamu na mengine kwenye kutoa huduma hiyo kutokana na kutofuata miongozo.


Hata hivyo aliishukuru Self kwa kuanzisha mafunzo hayo yatayowasaidia kuongeza uelewa na kuwapa elimu wakopaji kabla ya kuwakopesha na kuimarisha huduma za kifedha kwa kuondoa maneno ya uwepo wa mikopo chechefu na kuleta maendeleo yanayokusudiwa kwa jamii.  


Awali Meneja masoko na uhamasishaji wa Taasisi ya kiserikali ya utoaji Mikopo ya Self Microfinance Fund (Self MF) kutoka makao makuu Linda Mshana alisema lengo la kuzikutanisha taasisi hizo za kifedha ni endelevu ili kuzijengea uwezo kutokana na tatizo lililojitokeza baada ya tafiti kwenye Asasi hizo ikiwemo mikopo kutorejeshwa kwa wakati, uongozi na huduma bora kwa wateja na namna ya kupata wateja na mikopo kwa ajili ya wateja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com