WAVUVI HARAMU WAJISALIMISHA KWENYE KAMATI YA ULINZI NA USALAMA TANGA

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAVUVI wapatao 10 kati ya 17 waliokuwa wanajishuhulisha na uvuvi haramu wa kutumia mabomu wamejisalimisha mbele ya kamati ya ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga wakiwa pamoja na vifaa vyao walivyokuwa wakitumia. 

Walifikia uamuzi huo jana kufuatia agizo la mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Batilda Buriani ambalo lilitoa Juni 6, mwaka huu kwenye maadhimisho ya siku ya matumbawe la kuwataka wavuvi wanaovua kinyume na taratibu waweze kujisalimisha.

Wakati wakikabidhi hivyo, mkuu wa Mkoa huo Dkt. Batilda Buriani amesema baada ya kutafakari zaidi waliona wafuate mfumo wa jeshi la polisi, badala ya kukimbizana na wavuvi haramu ni bora kuwataka kwa hiyari yao kujisalimisha wenyewe.

Dkt Buriani amebainisha kwamba serikali ya awamu ya sita inalenga, viongozi kuwavuta na kuwaweka karibu wananchi wake na kujua matatizo yao ili kuyapatia ufumbuzi pale inapowezekana na endapo itsshindikana sheria zitafuata.

"Ni ukweli usiofichika kwamba Mkoa wa Tanga una bahati ya kuwepo kwenye ukanda wa bahari na kina takribani km 130, kwahiyo wengi waliozaliwa maeneo hayo bahari ndio mashamba yao na sisi tukiwa viongozi tunaangalia jinsi gani ya kuwasaidia kulima humo katika njia inayostahiki,

"Tukienda ndivyo sivyo, tutapata leo lakini kesho tutakosa na pia hicho tutakachokipata kutakuwa hakuna thamani kwamaana kitaleta madhara kiafya na pia tutakwenda kuua yale (matumbawe) mazalia ya viumbe wengi ndani ya bahari" amesema.

Akizungumza umuhimu wa matumbawe Dkt. Buriani amesema mbali na kuwa ni mazalia ya viumbe lakini pia yanazuia mmomonyoko wa ardhi ikiwa ni pamoja na maji ya chumvi kutoingia nchi kavu, lakini pia yanasaidua kunyonya chumvi baharini.

"Wengi wakio matumbawe wanamjua ni mawe tu ya baharini, lakini vile ni viumbe, yana manufaa makubwa, na ukiona sehemu miamba ya matumbawe imeshavunjwa ni lazima mmomonyoko wa ardhi utatokea,

"Matumbawe yana mchango mkubwa, na zaidi kuna viumbe aina tofauti wapatao 800 mazalia yao yapo katika matumbawe, kwahiyo mnapovua iwa kupiga mabomu mnaua hadi mayai ya samaki, na biashara yenu inakuwa siyo endelevu lakini pia faida yake siyo kubwa' amesema.

Hata hivyo amewataka wavuvi hao kwa kushirikiana pamoja na viongozi waliopo maeneo hayo kusaidia kusimamia uhifadhi na usimamizi wa bahari kwani chupa za plastiki zinazotupwa baharini kwa lengo la kuulia samaki, zikifika kule tayari ni uchafu kwakuwa haziozi.

"Hapa Tanga kwasasa tuna wavuvi takribani elfu 15, wadogo na wakubwa, na wengi ndio wapo kwenye uvuvi huu haramu, hivyo basi ninyi wenyewe ndio mtatusaidia kulindana na kuhamasishana kuachana na uvuvi haramu na kujisalimisha" amesisitiza.

Kwa upande wao wavuvi hao wamesema wameamua kujisalimisha baada ya kusikia agizo la mkuu wa Mkoa lakini pia zaidi ni kutokana na matatizo mengi waliyopata wakati wakifanya uvuvi haramu, ikiwa ni pamoja na kuziweka familia zao kwenye matatizo.

"Matatizo niliyopata mimi ni makubwa sana kiasi ambacho hata nikihadithia najiskia kulia, nusura nipoteze uhai wangu baada ya kukamatwa nikifanya uvuvi haramu, lakini sasa namuahidi mkuu wa Mkoa kwamba sitakaa nirudie tena na vifaa vyangu namkabidhi hapa" alisema Mwarabu Mustapha, maarufu kama Gebo, mkazi wa mtaa wa Mwarongo, kata ya Tongoni, jijini Tanga.

Mwenyekiti wa Kamati ya hifadhi mtaa wa Mwarongo Aboubakari Nundu amesema "baada ya maagizo ya mkuu, nilichukua uamuzi wa kwenda mtaani kwangu kwa hawa wenzangu ambao ni wahanga, nashkuru walinipokea na tukaelewana baada ya kuwahamasisha".

"Hawa waliopo mbele yako ni baadhi yao, walikuwepo 17 tulikuja nao lakini wameingia woga na kuondoka, niliwahakikishia usalama kwahiyo bila shaka mkuu tutaongea jambo hili Kwa amani na kila mmoja akatafute shughuli ya kufanya na kuendelea na maisha yake" amebainisha Nundu.

Mbali na hayo wavuvi hao wameiomba serikali kuwapatia vifaa ambayo vitafaa zaidi kuendeleza shuhuliz zao kwani uvuvi ndio kazi wanategemea kuendeshea maisha na familia zao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post