Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mkoa wa Kihuduma Makongo kuanza haraka kazi ya kuunganisha wananchi wa Kata ya Goba, mtaa wa Kibululu kwenye huduma ya majisafi ili kila mwananchi anufaike na uwekezaji uliofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kuboresha huduma ya majisafi.
Ametoa maagizo hayo kwenye mkutano wa wananchi wa Kata ya Goba, mtaa wa Kibululu akiwa kwenye siku ya pili ya ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa maji Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa wananchi ambao tayari wameshalipia kufanyiwa maunganisho ya maji wapewe haki yao ya maji, pasiwepo na ucheleweshwaji wowote.
"Ni haki ya kila mwananchi ambae ameshalipa gharama za maunganisho ya maji kupewa maji ndani ya siku saba za kazi na hii ni kulingana ma mkataba wa kisheria kati ya mteja na Serikali," ameeleza Mhe. Waziri.
Amesema kuwa Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi za kwenye huduma ya maji ili wananchi wanufaike na kazi kubwa inayofanywa na Serikali.
Mhe. Aweso amewataka Watumishi wanaohusika na usomaji wa mita kuwashirikisha wateja kwa ukaribu katika zoezi la usomaji mita ili kumsaidia mwananchi kujua kiwango halisi cha maji aliyotumia na kiasi cha fedha anachodaiwa.
"Usomaji wa mita shirikishi husaidia kupunguza au kuondoa malalamiko yanayoibuka mara kwa mara kutoka kwa wateja," amesema.
Ameongeza na kuwaelekeza Watumishi wa Mamlaka zote za Maji Nchini kutositisha huduma ya majisafi kwa wananchi kwa siku za sikukuu na wikiendi, kwa kuwa uhitaji wa maji huwa ni mkubwa kwa kipindi hicho.
Social Plugin