Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati alipofanya ziara katika ofisi za TBS Ubungo leo Julai 11, 2024 Jijini Dar es Salaam
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa utendaji mzuri na kulitaka kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara hususani upatikanaji wa alama ya ubora wa bidhaa ili kukuza biashara, kuongeza ajira, Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla.
Ameyasema hayo Julai 11, 2024, Ubungo jijini Dar es Salaam alipotembelea TBS kwa lengo la kufahamu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika hilo ili kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi wa Shirika hilo katika kuwahudumia wafanyabiashara.
Aidha, ametoa wito kwa Watumishi wa Shirika hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na ushirikiano baina yao pamoja na kuepuka kuwa kikwazo katika utoaji huduma kwa wafanyabiashara ili kuiwezesha sekta binafsi kukua kwa kasi na kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi shindani wa viwanda.
"Lengo la Wizara ya Viwanda na Biashara ni kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara zao kikamilifu, kuongeza ajira na kukuza Pato la Taifa kupitia Taasisi zake 13 ambazo tutaanza kuzipima kulingana na utendaji kazi wake". Amesema Dkt. Jafo.
Dkt. Jafo pia ameielekeza TBS kuhakikisha wajasiriamali wengi wanapata alama ya ubora na kufuatilia biashara hizo ili kuhakikisha kiwango cha ubora wa bidhaa hizo haushuki kwa ajili ya kuwalinda walaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amesema Shirika la viwango litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha bidhaa zinazouzwa nchini zinakidhi matakwa ya Viwango .

Social Plugin