WAZIRI JAFO APONGEZA UTENDAJI KAZI WA WAKALA WA VIPIMO

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo (WMA), eneo la Medeli jijini Dodoma, Julai 17, 2024.



· Ataka Taasisi nyingine ziige mfano wake

Na Veronica Simba – WMA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Selemani Jafo, amepongeza Wakala wa Vipimo (WMA) kwa utendaji kazi mahiri na wenye weledi na kutoa wito kwa Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara hiyo kuiga mfano wake.

Ametoa pongezi hizo mapema leo, Julai 17, 2024 jijini Dodoma alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Wakala huo, lililopo eneo la Medeli.

Mheshimiwa Jafo amekiri kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na utendaji kazi wa WMA kupitia ziara zake alizofanya kukagua kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Wakala huo, ambapo awali (Julai 11, 2024) alitembelea Kituo cha Uhakiki wa Vipimo kilichopo Misugusugu Mkoa wa Pwani na kujionea utendaji kazi wake.

“Kwa ujumla nimeridhishwa sana na utendaji wa Wakala huu na niwatake wengine waige mfano huu mzuri. Wito wangu, waendelee kufanya kazi kwa lengo la kuhakikisha Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inapata mafanikio makubwa katika maeneo yote,”amesema.

Ameongeza kusema kuwa, pongezi zake kwa Wataalamu wa Wakala wa Vipimo pia ni kutokana na kuonesha mfano mwema sana kwa kutumia mapato ya ndani, kujenga jengo hilo, hali inayothibitisha kuwa Taasisi hiyo ni miongoni mwa zile zinazofanya vizuri.

Akieleza zaidi, Waziri Jafo amesema lengo la ziara yake kukagua jengo hilo ilikuwa kujiridhisha kuhusu thamani ya fedha iliyowekezwa katika ujenzi huo pamoja na kasi ya utekelezaji wake ambapo kwa ujumla amesema ameridhishwa kwa kiasi kikubwa.

Akifafanua, amesema kuwa, kwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi, ambayo ni asilimia 81.5 anaamini jengo hilo linaweza kukamilika hata kabla ya muda uliopangwa ambao ni Januari 2025.

Hata hivyo, pamoja na kumpongeza Mkandarasi anayetekeleza ujenzi huo, Kampuni ya M/S Mohamed Builders chini ya Mshauri Elekezi, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), amewataka kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo kwa wakati na viwango stahiki kama inavyotarajiwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Jafo amewasisitiza watendaji wa WMA kuzingatia maelekezo aliyoyatoa kwao katika ziara yake ya awali, kuhusu kukagua maeneo yote yanayohusu ukaguzi hususani mita za umeme na maji kabla hazijafungwa kwa wateja ili kulinda haki za walaji ambao ni wananchi.

“Naelekeza mita zote za umeme na maji lazima zifikishwe Wakala wa Vipimo ili kuzipima kuangalia uthibiti wake kwa lengo la kuwapunguzia gharama wananchi. Isije mtu akafungiwa mita ambayo haina ubora, mwisho wa siku akalipa bili isiyo stahiki,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Joseph Maliti ametoa ahadi kwa Waziri kuwa Wakala utahakikisha maelekezo yake yote yanatekelezwa.

Naye Mwakilishi wa Mkandarasi, Mhandisi Justin Kyando amesema wana uhakika watakamilisha ujenzi kwa wakati kwani wako katika hatua za ukamilishaji.

Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma ulianza Julai 2, 2022 na unatarajiwa kukamilika Januari 2025 ambapo gharama yake ni shilingi bilioni 6.17.



Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo (WMA), eneo la Medeli jijini Dodoma, Julai 17, 2024.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo (WMA), eneo la Medeli jijini Dodoma, Julai 17, 2024.
Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Joseph Maliti akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) jijini Dodoma, wakati wa ziara ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo kukagua jingo hilo, Julai 17, 2024.
Mwakilishi wa Mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) jijini Dodoma, Kampuni ya M/S Mohamed Builders, Mhandisi Justin Kyando akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu maendeleo yake wakati wa ziara ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo kukagua jengo hilo, Julai 17, 2024.

Taswira ya jengo la Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) jijini Dodoma. Taswira hii imechukuliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, Julai 17, 2024.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo (WMA), baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Makao Makuu ya Wakala huo, eneo la Medeli, jijini Dodoma, Julai 17, 2024.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post