Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MAKAMBA AONGOZA KIKAO CHA MAWAZIRI 15 WA EAC


WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) ameongoza Mkutano wa faragha wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika Zanzibar.

Akizungumza katika Mkutano huo wa siku tatu ambao yeye ni mwenyekiti, Mhe. Makamba amesema Tanzania imejidhatiti kuhakikisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa imara, yenye umoja na inayofikia malengo yake.

“Madhumuni ya mkutano huu ni kuifanya familia yetu kuwa imara, kuifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza majukumu yake vizuri, Tanzania kama moja ya waanzilishi wa Jumuiya hii tumejidhatiti kuona jumuiya ikiwa na umoja, imara na yenye kufanikiwa” alisema Mhe. Makamba

Naye Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Musalia Mudavadi ameipongeza Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuongeza kuwa ni wakati muafaka kwa nchi wanachama kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali ndani ya jumuiya kwa manufaa ya wananchi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kupongeza juhudi za kuimarisha jumuiya.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri Mhe. Deng Alor Kuol amesema kufanyika kwa mkutano huo ni jambo jema hasa ikizingatiwa kuwa utaangalia masuala ya amani, usalama na mtangamano wa jumuiya ikiwa ni hatua za kuifanya jumuiya kusonga mbele.

Mkutano huo wa faragha unajadili taarifa ya Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya; hali ya amani, usalama, siasa na uhusiano kati ya nchi wanachama; kutathmini na kujadili mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na masuala yanayokwamisha ufikiwaji wa malengo ya programu na miradi inayopangwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com