WIZARA YA MADINI, KAMPUNI YA FARU GRAPHITE WAJADILI MAENDELEO YA MRADI


Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo Julai 5, 2024 aliongoza kikao kati ya Wizara na Kampuni ya Faru Graphite Corporation kilicholenga kujadili maendeleo ya mradi wa uchimbaji madini ya Kinywe (graphite)  katika eneo la Mahenge Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika  jijini Dodoma, Mbibo aliihakikishia kampuni hiyo kushughulikia changamoto inazokabiliana nazo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinazohusika moja kwa moja  na masuala yatakayowezesha utekelezwaji wa mradi husika ili kuuwezesha kutekelezwa kwa wakati.

 Faru Graphite corporation ni kampuni ya ubia kati yake na Serikali ya Tanzania ambapo Serikali ina umiliki wa hisa zisizofifishwa za asilimia 16 na kampuni ya Black Rock Limited yenye hisa asilimia 84

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Faru Graphite Corporation John de Vries alieleza kwamba, katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kampuni hiyo imeweza kushughulia masuala muhimu ikiwemo upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa mradi ili kuhakikisha unatekelezwa kwa wakati.

Pia, de Vries alitumia fursa hiyo kuishukuru Wizara ya Madini kwa ushirikiano inaoutoa katika kutatua changamoto zinazoikabili, na kuongeza kwamba, Wizara imesaidia kufikia makubaliano kati ya kampuni hiyo na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ya ujenzi wa miundombinu na usambazaji wa umeme katika eneo la mradi.

#InvestInTanzaniaMiningSector

#Vision2030: MadiniMaisha&Utajiri

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post