Mwanamke wa miaka 31 kutoka kijiji cha Mugamba-ciura katika kaunti ndogo ya Mwea-Mashariki nchini Kenya anaomba usaidizi wa kutafuta sindano ya cherehani kwenye koo lake.
Kufuatia tukio hilo, familia yake na majirani wamesikitika, kwani hakuna hospitali iliyofanikiwa kupata na kuitoa sindano hiyo.
“Hii ni wiki ya nne na sindano bado iko kooni. Hospitali zinaomba KSh 10,000 ili kuitafuta sindano hiyo, lakini hatuwezi kumudu hiyo gharama. Tunatatizika kulisha familia yetu na mke wangu anaendelea kuteseka," Kelvin Maina, mumewe, aliambia Citizen Digital.
"Tutampoteza kwa kukosa pesa, licha ya kuwa na viongozi waliochaguliwa katika mkoa huu?" jirani mmoja alisikika akishangaa.
Kwa nini familia ya Kirinyaga inaomba msaada?
Mama huyo wa watoto wanne, ambaye pia anamnyonyesha mtoto wake wa miezi minane, anapata shida kubwa ya kula kwa sababu ya kuwepo kwa sindano hiyo mwilini.
Baada ya kutembelea Hospitali ya Embu Level 5 na Hospitali ya Kerugoya Level 4, walipewa rufaa ya kwenda kwenye tasisi ya matibabu ya kibinafsi kutafuta usaidizi zaidi, ambapo hawakuweza kumudu.
"Baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Kerugoya hadi kituo cha kibinafsi, hawakuweza kuendelea kwa sababu hawakuweza kumudu huduma hizo. Inatisha kwamba hospitali ya Level 4 haikuweza kushughulikia dharura hii," David Karatai alisema.