Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Akizungumzia maandalizi ya Mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani amesema mikutano hiyo na wadau wa uchaguzi inalenga kupeana taarifa mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya kuanza rasmi kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari.
“Lengo hasa la kukutana na wadau hawa ni kupeana taarifa za uwepo wa zoezi hili na kuwapitisha katika vifaa na mifumo ya uandikishaji pamoja na kuona namna zoezi litakavyofanyika vituoni. Aidha,tutapeana taarifa juu ya maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na maandalizi hayo pamoja na mambo mengine yanajumuisha uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura, uboreshaji wa majaribio, ununuzi wa vifaa na ushirikishwaji wa wadau kama ambavyo itafanyika kesho katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga,”amesema Kailima.
Amewataja wadau watakao shiriki mikutano hiyo ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila na wote ni kutoka mikoa husika.
Aidha, katika mikutano hiyo kutakuwa na mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi mada itakayozungumzia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Wataalamu wa TEHAMA watawapitisha kwenye mfumo wa uandikishaji na vifaa vitakavyotumika.
Katika Mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi itagusia masuala mbalimbali ikiwepo uzinduzi wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari, Uboreshaji wa Daftari,Wasio na sifa za kuandikishwa,Idadi ya wapiga kura wanaotarajiwa kuandikishwa, Maandalizi ya uboreshaji wa Daftari, Mafunzo kwa watendaji wa uboreshaji, Ushirikishwaji wa wadau, Taasisi na Asasi pamoja na Mchango wa wadau katika kufanikisha zoezi la uboreshaji.
Tume tayari imeanza zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo uzinduzi ulifanyika mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024 na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB). Uzinduzi huo ulienda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi.
Aidha, mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaendelea sasa katika mikoa ya Kagera na Geita ambapo uboreshaji ulianza tarehe 5 hadi 11 Agosti, 2024.
Social Plugin