Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Mwenyekiti Tawi la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kata ya Masekelo Wilaya ya Shinyanga Mjini Bi. Amina Francis Mwandu amewataka Wanawake wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura ambalo mkoani Shinyanga linatarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 21 - 27,2024 huku akiwahamasisha kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.
Amina ametoa rai hiyo leo Jumatatu Agosti 19,2024 wakati akizungumza na Wanawake wa Chama cha Mapinduzi na wananchi wa kata ya Masekelo ambapo ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye vituo ili kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.
"Wananchi wote mnaombwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kupiga kura, kugombea na kushiriki katika Uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024 ili kupata viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo ya nchi yetu, Wanawake msibaki nyuma, jitokezeni kwa wingi kugombea nafasi za uongozi",amesema Amina.
"Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Shinyanga utafanyika kuanzia tarehe 21 hadi 27, Agosti, 2024, vituo vitafunguliwa saa 02:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni, naomba tutumie fursa hii kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura. Kauli mbiu ni 'Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora', amesema.
"Naomba pia akina Mama mjitokeze kwa wingi kujisajili kwenye Umoja wa Wanawake (UWT) kwa mfumo wa Kielektroniki ili kuwa Wana Chama hai wa UWT na pia kulipia ada za uanachama wa CCM, na wale ambao bado hawajajiunga CCM tunawakaribisha sana kujiunga",ameongeza Amina.
Kwa Mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa Mkoa wa Shinyanga, Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 209,951 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 ya wapiga kura 995,918 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ambapo Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Shinyanga utakuwa na wapiga kura 1,205,869.
Vituo 40,126 vya kuandikisha wapiga kura vitatumika katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2024 ambapo kwa Mkoa wa Shinyanga kuna vituo 1,339 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 122 katika vituo 1,217 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
Mwenyekiti Tawi la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kata ya Masekelo Wilaya ya Shinyanga Mjini Bi. Amina Francis Mwandu akizungumza kwenye mkutano
Mwenyekiti Tawi la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kata ya Masekelo Wilaya ya Shinyanga Mjini Bi. Amina Francis Mwandu akizungumza kwenye mkutano
Mwenyekiti Tawi la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kata ya Masekelo Wilaya ya Shinyanga Mjini Bi. Amina Francis Mwandu akizungumza kwenye mkutano
Social Plugin