MRADI WA MAJI WA BILIONI 40 WAANZA KUTEKELEZWA MUHEZA


Na Hadija Bagasha Muheza

MRADI wa maji wa miji 28 wilayani Muheza mkoani Tanga, utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 40, umeanza kutekelezwa kwa kuchimbwa matenki mawili makubwa.

Aidha, akitembelea kukagua uanzaji wa mradi huo, mbunge wa Muheza na Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma almaarufu MwanaFA, alisema mradi huo utakuwa muarobaini wa kumaliza tatizo la maji.

MwanaFA alisema anamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusaini mkataba wa kutekelezwa mradi huo Ili kuwezeaha upatikanaji wa maji katika miji hiyo Muheza ukiwemo hatua ambayo ni ya kumpongeza.

"Fedha hizi bilioni 40 kama hazitaweza kumaliza tatizo la maji wilayani Muheza basi kero ya maji haiwezi kuisha tena," alisema.

MwanaFA alitembelea eneo la Kilulu kunakojengwa tenki kubwa la kuhifadhi maji, kukagua tenki la eneo la NHC na Kwamkabala ambako wananchi waliokuwa wakichota maji walimpongeza mbunge huyo kutokana na kupungua makali ya upatikanaji wa maji Muheza.

Mbunge huyo alisema wakati akiingia kuwa mbunge wa Jimbo hilo, hakukuwa na maji na ndiyo hasa kulikomsukuma kugombea Ubunge Ili asaidiane na wananchi kuondoka kero hiyo ambapo wananchi wanapata maji kwa kwenye vilula vinavyotoa maji mara tatu Kwa wilki.

Msimamizi wa mradi wa maji wa miji 28 Andrew Shilinde alisema wameanza mradi huo kwa kujenga matenki mawili katika maeneo ya Kilulu na Kwafungo.

"Tenki hili la Kilulu litakuwa na ujazo wa lita milioni 2 na lile la Kwafungo ambalo limeanza kujengwa kuanzia Julai litakuwa na ujazo wa lita laki tano," alisema.

Shilinde alisema ujenzi wa matenki hayo utakamilika Juni mwakani, mradi utakamilika Desemba mwakani ambapo wananchi wa Muheza watakuwa wakipata maji masaa 24.

Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga-Uwasa wilayani Muheza, Mhandisi Ramadhani Nyambuka alisema kwasasa hali ya upatikanaji wa maji Muheza ni wastani wa asilimia 73 wananchi wanapata maji tofauti na mwaka 2020.

Alisema upatikanaji huo kwa kiasi kikubwa umetokana na juhudi za mbunge MwanaFA ambaye alimleta Katibu Mkuu wa Wizara ya maji ambaye alileta shilingi milioni 700 na baadae milioni 400 ambazo ziliboresha hali ya upatikanaji wa maji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post