MWENGE WA UHURU WARIDHISHWA NA UENDELEVU WA MRADI WA MAJI UNAOTEKELEZWA NA SHUWASA BUGAYAMBELELE


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na hatua zilizopigwa katika uendelevu wa mradi wa maji safi na salama kwenye kijiji cha Bugayambelele, Manispaa ya Shinyanga.

Mradi huu, unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), ulizinduliwa mwaka 2023 kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa maji safi kwa wananchi.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Eliakimu Mnzava, baada ya kutembelea na kukagua mradi huo leo Jumapili Agosti 11,2024 ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo yaliyofikiwa.

Ametumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya maji, akibainisha kuwa serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wote.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Eliakimu Mnzava.

Mnzava ameipongeza SHUWASA kwa uendelevu wa mradi huo na kuwasihi wananchi kuendelea kulinda miundombinu hiyo.

“Ni muhimu kwa wananchi kuzingatia jukumu lao la kulinda miundombinu hii ili kuhakikisha malengo ya serikali yanatimia, na kila mmoja apate maji safi na salama kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Shinyanga, Angel Mwaipopo, akisoma taarifa ya uendelevu wa mradi huo kwa kiongozi wa Mwenge, ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 10,165.

“Mradi huu umesababisha ongezeko la upatikanaji wa maji kwa kaya kutoka asilimia 35 hadi asilimia 60, huku idadi ya kaya zinazopata huduma ya maji ikiongezeka kutoka 142 hadi 248,” amesema Mwaipopo.
Mradi huu ulisanifiwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Shinyanga kwa kuongeza mtandao wa maji kwa kilomita 8.041, ambapo RUWASA ilijenga kilomita 1.5 na SHUWASA ikajenga kilomita 6.459.

“Mradi huu umewezesha pia ujenzi wa Gati (Water Kiosk) moja ambalo linahudumia zaidi ya kaya 30 kwa nyakati tofauti,”

Amesema kuwa SHUWASA inapanga kuongeza mtandao wa majisafi kwa kilomita 2.1 zaidi katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuwafikia wakazi wengi zaidi.

Thamani ya mradi huo ni shilingi 279,465,134.40, ikiwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Wananchi wa Shinyanga wameendelea kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kutekeleza miradi ya maji ambayo imepunguza adha ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Mbio za Mwenge wa Uhuru zinaendelea katika Manispaa ya Shinyanga, ambapo Mwenge utapita katika miradi kumi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 4.2, huku ukikimbizwa kwa umbali wa kilomita 74.5.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Shinyanga, Angel Mwaipopo, akisoma taarifa ya uendelevu wa mradi huo kwa kiongozi wa Mwenge leo Jumapili Agosti 11,2024. 
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Eliakimu Mnzava, akiipongeza SHUWASA kwa uendelevu mzuri wa mradi wa maji Bugayambelele Manispaa ya Shinyanga.
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Shinyanga SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola awali akielezea mradi huo unavyowanufaisha wakazi wa kata ya Kizumbi na maeneo jirani katika Manispaa ya Shinyanga.
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Shinyanga SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola awali akielezea umuhimu wa mradi huo kwa wakazi wa kata ya Kizumbi.
Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini ambaye ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Paschal Katambi akizungumza.Mwonekano katika mradi wa maji Bugayambelele kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga.

Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
Watumishi wa SHUWASA wakiwa kwenye picha ya pamoja na mkurugenzi mtendaji wa mamlaka hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post