Mkurugenzi mkuu wa TAFORI Dk. Revocatus Mushumbusi akiangalia moja ya mizinga ya nyuki wadogo na wasiouma katika maonesho ya wakulima 88 kanda ya mashariki mkoani Morogoro.
Mkurugenzi mkuu wa TAFORI Dk. Revocatus Mushumbusi akipokea maelekezo ya umuhimu wa asali katika banda la TAFORI kwenye maonesho ya kilimo 88 kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Morogoro
Na Christina Cosmas, Morogoro
WAKULIMA nchini wametakiwa kufuga nyuki kwenye mashamba ya chakula wanayolima ili kuondokana na ukosefu wa maeneo ya kufugia wakidhani nyuki hufugwa kwenye misitu mikubwa pekee.
Hayo yamesemwa na Mkurugezi Mkuu wa Taasisi ya utafiti wa misitu Tanzania (TAFORI) Dk. Revocatus Mushumbusi kwenye sherehe za maonesho ya wakulima 88 kanda ya mashariki yaliyofanyika mkoa wa Morogoro.
Dk. Mushumbusi anasema watu wamezoea kufanya ufugaji wa nyuki kupitia à misitu mikubwa lakini tafiti walizofanya zimeonesha kuwa hata kwenye mashamba ya chakula wana uwezo wa kupata mazao yatokanayo na nyuki kwa kiasi kikubwa hadi kufikia kupata si chini ya kilo 19 hadi 23 kwenye mzinga mmoja kwa wakati mmoja.
Naye Mtafiti kutoka TAFORI Stanslauss Lukiko anawataka wakulima kutotumia viuatilifu ambavyo vinawadhuru nyuki bali watumie nyuki kwa ajili ya uchavushaji na kupata mazao mengi ambapo uchavushaji unafanya mbegu pamoja na mazao kuvunwa yakiwa mengi na yenye ubora.
Alisema TAFORI inaendelea na tafiti za kimkakati ikiwemo utafiti wa kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya ufugaji nyuki inayofanyika Wilayani Kongwa jijini Dodoma ili kukabiliwa na changamoto hiyo na kuwaondoa kwenye dhana ya kuwa maeneo ya kufugia ni msituni pekee huku misitu hiyo ikiwa mbali na maeneo wanayokaa.
Lukoki anasema katika utafiti huo wa kimkakati wamejaribu kuweka majaribio kwenye maeneo yenye mashamba yasiyotumia viuatilifu na kuona kuwa kuna faida zinazopatikana ikiwemo uchavushaji wa mazao na kupata asali sambamba na mazao mengine ya nyuki.