Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NGAMIA 300 WAKAMATWA MPAKANI MWA TANZANIA NA KENYA


Na Hadija Bagasha Tanga.

NGAMIA 300 wamekamatwa kwenye hifadhi ya msitu wa Mwakijembe uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, wakichungwa kwa lengo la kupata malisho.

Ngamia hao wamekamatwa Julai 23 mwaka huu katika msitu huo wamebaki watatu baada ya wengine kutoroshwa.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian ameyasema hayo wakati alipotembelea mnada wa mifugo wa kimataifa uliopo eneo la mpakani Horohoro kwa ajili ya ukaguzi wa mnada huo na kueleza kuwa ngamia hao ambao wameingia mpakani hapo kutokea nchi jirani ya Kenya wapo chini ya ulinzi maalum hadi pale taratibu za kisheria zitakapokamilishwa ili kuruhusu ngamia hao kuchukuliwa na mmiliki kutoka Kenya kutokana na uharibifu uliofanywa na ngamia hao katika misitu ya TFS pamoja na misitu ya kijiji.

Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian alisema mfugaji aliyekamatwa akiwa na mifugo hiyo aliachiwa kutokana na ujirani mwema lakini mifugo hiyo alitakiwa ailipie Kwa Sheria ya TFS kutokana na ngamia hao kufanya uharibifu huo.
"Ngamia hawa wamekuwa wakiingizwa kupitia njia za panya kula malisho katika eneo letu na hao walikuwa 300 kwa ujirani mwema tumeendelea kuachia lakini sasa tumeona huwezi ukaingiza mifugo ama ukiwa mtanzania huruhusiwi kuingiza mifugo kwenye hifadhi ya misitu ya TFS na hata katika misitu ya kijiji baada ya kuwaona wako kwa siku 4 nzima jitihada za kuwaondoa zimeshindikana ilibidi sisi tuwashike mheshimiwa DC amefanya mawasiliano na wenzake wa Lungalunga tulimkamata mfugaji lakini tulimwachia kwa ajili ya ujirani mwema",alisema Batilda.

"Hawa mifugo tumeona kulingana na sheria zetu za kuingiza mifugo kwenye hifadhi ya misitu kuna faini ambayo hata mtanzania anatozwa ukiharibu uoto wa asili kuna faini yake yule mfugo tu kuingia ndani kuna faini yake mtu anayefuga kuingia ndani kuna faini yake na hivyo vyote lakini pamoja na gharama ya kuwalisha wale mifugo kuna gharama zake kwa hiyo Halmashauri imetengeneza gharama inayoingia kwenye gharama ya Halmashauri za Serikali tumempatia mfugaji aweze kuturejeshea gharama zile na kulipa faini zile za TFS ndio maana mnawaona hawa mifugo hapa, "alisema Batilda.

Aidha akizungumza mara baada ya kukagua mnada wa Kimataifa wa Horohoro Mkuu wa Mkoa Batilda ameagiza wataalamu wa sekta ya mifugo kupitia mpango wa utoaji vibali vya kusafirisha mifugo nje ya nchi ili kulinusuru soko jipya la kimataifa lililojengwa ambalo kwa sasa halitumiki ipasavyo kutokana na wafanyabiashara wengi kulikwepa na kutumia mpango wa vibali na kulikosesha Taifa mapato.

"Suala zima la dhana ya kuwepo kwa mnada huu wa kimataifa ni kuhakikisha kwamba mifugo yetu wawe Ng'ombe, Mbuzi, kondoo wanapigwa mnada hapa na sio eneo la kukatisha kibali cha kusafirisha mifugo nje ndio maana tukajenga na kilinge ili Ng'ombe akifika kwenye mizani apimwe aingie kwenye kilinge tumchague kwamba Ng'ombe huyu atauzwa kwa kiasi gani sasa ivi ananunuliwa kwenye soko la awali la pili akija hapa tunamkatia kibali cha kusafirisha nje sio madhumuni ya mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan", alisisitiza Batilda.


"Mheshimiwa Rais alikusudia soko hili litumike wafugaji wapate bei nzuri waende wakauze kule wapate fedha zao nzuri na sisi tumekubaliana na Halmashauri zetu tuchukue fursa hii vijana wetu waanze BBT mifugo na bahati nzuri tuna BBT mifugo kitaifa hapa Tanga wanakuja vijana kutoka Tanzania nzima tumemuomba Waziri tuweke vijana wetu 30 maadamu BBT mifugo ipo hapa Tanga vijana wetu hawatakuwa na gharama kwasababu wanaishi hapa hapa Tanga", aliongeza  Batilda.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Gilbert Kalima ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote ya Mkuu wa Mkoa huku akimuomba aongeze msisitizo Wizarani ili suala la soko la mazao ambalo limetengewa eneo lipewe kipaumbele ili jamii iweze kulitumia na hatimaye kuimarisha uchumi wao.

Naye Mwenyekiti serikali ya Horohoro kijijini Jumapili Yohana amesema matarajio ya wananchi kwenye mnada huo ni kwamba mnada huo uwe ni soko la kimataifa wanyama wote ikiwemo mbuzi, kondoo, Ng'ombe wapelekwe mnadani hapo wananchi wajumuike kwa pamoja kufanya mnada na hatimaye serikali ipate mapato yake tofauti na ilivyo sasa.


Mnada wa mpakani Horohoro ulianza kufanya kazi Septemba 3 mwaka 2023 ambapo mpaka sasa jumla ya minada 49 imekwisha kufanyika ambapo katika kipindi cha miezi 11 jumla ya mifugo 7503 iliingia mnadani ikiwa Ng'ombe 6105 na mbuzi 1398 jumla ya Ng'ombe 4393 na Mbuzi na Kondoo 953 waliuzwa kati ya hao Ng'ombe 1556 Mbuzi na kondoo 263 waliuzwa nje ya nchi na kupata kiasi cha shilingi milioni 44.3 ziliingia kupitia Pos ya mnadani.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com