Mkurugenzi mkuu wa TSB, Saddy Kambona
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Mkonge nchini (TSB) Saddy Kambona ametoa ufafanuzi kuhusiana na habari zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti ambayo yaligusa sekta hiyo hususani wakulima wadogo wa zao la mkonge.
Kambona amebainisha kwamba magazeti hayo yalichapishwa kuhusu Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) vya Hale, Magoma, Magunga, Mgombezi na Mwelya vilivyopo Wilaya ya Korogwe.
Ametaja gazeti la Raia Mwema la julai 24 - 30 ambalo lilichapisha kichwa cha habari 'Kinachoenfelea kwenye Mkonge, utamwaga machozi', lakini siku julai 26 na 30 gazeti la Tanzania Leo lilichapisha habari kwamba 'Kinachoendelea kwenye Mkonge ni ukatili kwa wakulima: Serikali iingilie kati garama za usindikaji na julai 30 na Agost 05 gazeti la Jamhuri lilichapisha kichwa cha habari 'Bashe 'ishu' ya Mkonge unaiwez'.
Sadi amefafanua kuwa mambo yaliyo yaliyoguswa na waandishi wa habari hizo ni Kampuni ya Sisalana kupandusha bei ya huduma ya uchakataji kutoka sh milioni 1 kwa tani hadi sh milioni 1.25 kwa tani, uchakavu wa mitambo ya uchakataji wa Mkonge yanayomilikiwa na Sisalana (T) Ltd unaosababisha hasara kwa wakulima.
"Ufafanuzi wa Bodi ya Mkonge ambao ni msimamizi wa sekta ndogo ya Mkonge, hoja hii ni ya kweli, julai 14 tulipokea barua kutoka Sisalana kuhusu kufanya maboresho na kati ya moja wapo lilikuwepo hili la kupandisha bei, TSB ilisubiri jibu la AMCOS kuhusiana na hoja za kanuni ya Sisalana,
"Lakini Julai 15 AMCOS waliandika barua kuomba TSB miongozo wa bei ya usindikaji baada ya kupokea hati za madai ya malipo zenye bei mpya ya usindikaji lakini TSB ilielekeza uongozi wa AMCOS kutolipa ankara hizo mpaka pale suala hilo lipatiwe ufumbuzi na kuamuliwa kwa pamoja baina ya Bodi na Sisalana" alibainisha.
Kwa upande wa uchakavu wa majengo, Kambona amekiri kuwa ni chakavu kwakuwa ni ya zamani tangu enzi za mkoloni lakini ni bora na yenye ufanisi mzuri katika kuzalisha singa bora kuliko sehemu kubwa ya mitambo ya kisasa.
Amefafanua kwamba makampuni yote makubwa ya Mkonge kama Amboni Plantation ltd, Mohamed Enterprises ltd, Highland Estates yanatumia makotona sawa na Sisalana lakini tofauti ni matunzo, usimamizi na uendeshaji wake.
"Mitambo ya Sisalana ikifanyiwa matengenezo vizuri kama inavyofanyika kwa makampuni ya wakulima wakiwa na kuweka katika ulingano sawa ina uwezo wa kufanya vizuri zaidi na kupunguza hasara ya kutupa singa za wakulima shimoni,
"Natoa wito kwa kampuni ya Sisalana, matengenezo ya haraka ya mitambo yake hasa katika mashamba ya Magoma, Mwelya na Ngombezi, kwa maana hali ya mitambo ya mashamba ya Hale na Magunga ina nafuu" amesisitiza.
Kambona alisema suala la ununuzi wa Mkonge na matatizo yake ni kwamba tangu mwaka 2021 kampuni ya Mohamed Enterprises ltd (MeTL) ilinunua Mkonge kwa miaka mitatu mfululizo na mkataba uliisha Agosti 2023 na haikuongeza mkataba ndio TSB ilipoitisha zabuni ya ununuzi.
Amebainisha kwamba kampuni ya WEFARMTZ ilishinda zabuni kwa bei ya sh milioni 3.9 na kuanza kununua Mkonge wa AMCOS hadi Aprili 22, 2024 ambapo mkataba ulivynjika kutokana na ukiukwaji wa vipengele vya mkataba.
Amesema baada ya kuvunjika kwa mkataba huo, mshindi wa pili kampuni ya Agriculture Fibers ilisaini mkataba April 22 kwa bei ya mshindi wa kwaza na ndiyo inayoendelea mpaka sasa.
"Hata hivyo,TSB kwa kushirikisha ana na AMCOS pamoja na Wizara ya Kilimo tumepambana Kuretea maslahi ya mkulima mdogo kwa kulinda bei ya Mkonge isiporomoke, serikali inatumia nguvu nyingi kukuza kilimo hiki, bei nzuri ya Mkonge ni kivutio muhimu,
"Hatuwezi kuruhusu jitihada za serikali za kuongeza uzalishaji wa Mkonge kufikia tani 120,000 ifikapo 2025/26 zikwamishwe kwa kuweka mazingira ya kuwakatisha tamaa wakulima ya kuendeleza kilimo hiki, kilimo ni biashara na tutahakikisha mkulima mdogo ananufaika" amesisitiza.
Vilevile amesema kuhusu suala la umiliki wa makotona baina ya NSSF na AMCOS kwa uwiano wa asilimia 60 kwa 40 mtawalia, lilianza kufanyiwa kazi tangu 2022/22 ambapo TSB, AMCOS pamoja na Sisalana zilikutana na Msajili wa hazina na kujadili.