Kaimu Mkurugenzi wa PACESH, John Shija akitoa tamko la kulaani kitendo cha ubakaji na ulawiti alichofanyiwa msichana anayedaiwa kuwa ni mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kituo cha Huduma ya Msaada wa Kisheria Mkoa wa Shinyanga (PACESHI) kimeungana na makundi yote yaliyoshiriki kulaani kitendo cha ubakaji na ulawiti alichofanyiwa msichana anayedaiwa kuwa ni mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
Agosti 4, 2024 zilisambaa video katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo, huku wakimtuhumu kwa kile kilichosikika katika video hiyo kuwa ametembea na mume wa mtu.
Kadhalika, katika video hiyo inayodaiwa kuchukuliwa na vijana hao, binti huyo alisikika akieleza anakotokea na kumwomba msamaha mtu aliyetambulishwa kwa jina la afande.
Kufuatia tukio hilo, Kituo hicho kinachotoa msaada wa kisheria mkoani vyombo vyote vinavyopaswa kushughulikia jambo hilo vihakikishe vinatimiza wajibu wake kikamilifu na asiwepo mtu wa kukalia, kuchezea na kufumbia macho haki stahiki.
Akisoma tamko la kulaani tukio hilo leo Agosti 9,2024, Kaimu Mkurugenzi wa PACESH, John Shija amesema kwa masikitiko makubwa watoa huduma na wasaidizi wa kisheria Mkoa wa Shinyanga wameumizwa sana kwa kitendo kilichosababishwa kusambaa kwa video ya binti ambaye amefanyiwa ukatili mkubwa ikijumuisha ubakaji na ulawiti uliofanywa na vijana wanaosadikiwa kuwa watano kwa maelekezo maalumu kutoka kwa mmoja wa wanawake kama sehemu ya adhabu kwa kuwa anatembea na mume wake.
"Video hiyo ambayo imeanza kusambaa tangu tarehe 3/8/2024 ikionyesha kuwa Kitendo hicho kimetendeka jijini Dar es Salaam wilaya ya Temeke mtaa wa Yombo kimehusisha baadhi ya watu waliotenda kosa hilo ni watumishi wa baadhi ya majeshi yetu hapa nchini Tanzania",amesema Shija.
"Kitendo hicho si cha kulaani tu bali ni cha kukemea vikali na kuchukuliwa hatua kali za kisheria, kwakuwa kitendo hicho kimekwenda kinyume cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya 1977, ibara ya 5 (c) na (e) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai sura ya 20 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2022 kwa kuwa matendo yote hayo yamejinaishwa na sheria hiyo, sambamba na hilo sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyorekebishwa 2022 katika kif cha 31 kinatoa adhabu kwa watenda makosa ya ubakaji wa kundi.
Sambamba na hilo vitendo hivyo vinafedhehesha nchi kwa kuwa kama nchi tumejinasibu kulinda haki za binadamu dhidi ya ukatili, udhalilishaji, na pia tunanyong’onyesha jitihada za nchi chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ameanzisha mikakati mbalimbali ya kushughulikia ukatili wa kijinsia ikiwemo Kampeni ya Huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid Campaign",ameeleza Shija.
Amebainisha kuwa, vitendo hivyo vimetendwa si kwa bahati mbaya bali vina dhamira ya dhati, kuvunja katiba, sera za nchi na jitihada za nchi pamoja na viongozi wake, kwa kuwa waliofanya vitendo hivi ni watu wenye uelewa wa sheria hizo.
Kaimu Mkurugenzi wa PACESH, John Shija akitoa tamko la kulaani kitendo cha ubakaji na ulawiti alichofanyiwa msichana anayedaiwa kuwa ni mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
Social Plugin