Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTO MIRONGO UNAVYOCHANGIA UCHAFUZI WA MAZINGIRA YA ZIWA VICTORIA


 Na Obunde Michael - Mwanza

Mto Mirongo ni miongoni mwa mito inayochangia uchafuzi wa mazingira ya ziwa Victoria.

Mto huo unaopita katikati ya Jiji la Mwanza kwa muda mrefu umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi za uchafuzi wa mazingira hususani maji machafu kutoka kwenye viwanda pamoja na makazi ya watu.

Maji taka yanayotiririshwa kupitia mto huo huwa na kemikali,taka ngumu pamoja na na vitu vingine vyenye sumu vinavyosababisha uchafuzi wa maji.

Eneo la kando ya mto Mirongo limeathirika na mmomonyoko wa ardhi, jambo linalopelekea mchanga mwingi kuingia mtoni na kufanya maji kuwa na matope na kushuka ubora wake.

Kandokando mwa mto pia kuna shughuli za kilimo ambazo husababisha mbolea na madawa ya kuulia wadudu kumwagika kwenye maji na kuathiri afya ya viumbe wa majini, watumiaji maji ya mto huo pamoja na ziwa victoria.

Ongezeko la uchafuzi wa mazingira unachangiwa zaidi na mto mirongo kugeuzwa kama dampo la taka ngumu kama vile za plastiki,mabaki ya vyakula na taka nyinginezo,jambo ambalo linaathiri ubora wa maji na afya ya viumbe wa majini.

Akizungumzia changamoto hiyo,Mwenyekiti wa serikali ya mtaa ya Rufiji Abdlahi Mbaraka amesema kuwa utupaji ovyo wa taka zikiwemo za plastic pamoja na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye kingo za mto mirongo umechangia mto mirongo kuwa dampo la taka.

Naye mwenyekiti wa kamati ya mazingira kata ya Mirongo 
Badrudin Subuga amesema elimu ya utunzaji wa mazingira inayotolewa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali bado haijazaa matunda kutokana na mwamko mdogo wa baadhi ya wafanyabiashara ndogondogo katika suala la usafi.

Diwani wa kata ya mirongo Hamidu Suleiman amesema kuwa halmashauri ya jiji la mwanza inakusudia kuboresha mazingira ya mto huo kwa kujenga kingo zake pamoja na kuongeza kina zake ambapo usanifu wa mradi huo tayari umekamilika na kinachosubiriwa ni kuanza kwa utekelezaji wake wa mradi huo.

Kwa upande wake, Afisa mazingira wa halmashauri ya Jiji la Mwanza  Fanuel Kasenene amesema kuwa udhibiti wa taka zikiwemo za plastiki , kielektroniki pamoja na taka za hospitali umekuwa mgumu na kuchangia taka hizo kwenda moja kwa moja kwenye ziwa Victoria.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Kasenene ameiasa jamii kujiepusha na vitendo vya uharibifu wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo zimeanza kushuhudiwa katika bonde la ziwa Victoria ikiwemo ukame pamoja na kupungua kwa samaki.

Septemba Mwaka Juzi,Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango  akiweka Jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji alieleza kukerwa na ongezeko la taka za plastic zinazoingia kwenye ziwa Victoria kupitia mto huo na kuuagiza uongozi wa mkoa wa mwanza kuimarisha utunzaji wa mazingira ili kulinda chanzo cha maji safi ambacho ni ziwa Victoria,agizo ambalo halijatekelezwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com