BASHUNGWA ATOA WITO KWA WATANZANIA KUJITOKEZA UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA

Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa watanzania wenye sifa za kujiandikisha katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza katika vituo ili kupata Kitambulisho cha Mpiga Kura kitakachowawezesha kupata haki ya kuchagua Viongozi katika Uchaguzi.
Bashungwa ametoa wito huo leo Agosti 09, 2024 mara baada ya kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kituo cha Shule ya Msingi ya Ahakishaka, Kata ya Nyabiyonza Wilayani Karagwe Mkoani Kagera.

“Tukitaka kupata viongozi wazuri hatua ya kwanza ya kufanya ni kujiandikisha kwenye daftari ili tuweze kutumia haki yetu ya kidemokrasia muda utakapofika wa uchaguzi”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuboresha zoezi hilo na kufanya kazi kwa weledi inayoimarisha Demokrasia nchini.
Aidha, Bashungwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuendelea kuimarisha Demokrasia nchini na kuendelea kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Naye, Bw. Fidelis Makata, Mwandikishaji wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kituo cha Ahakishaka, ameeleza kuwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linafanyika kwa siku saba kuanzai tarehe 05 hadi 11 Agosti 2024.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea unaongozwa na kauli mbiu “Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora”.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post