AWESO AOMBA BOTI PANGANI KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI


Na Hadija Bagasha Tanga, 

Waziri wa maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani Jumaa Aweso ameiomba serikali kuwapatia usafiri wa  boti ya kisasa zinazokwenda kasi katika wilaya hiyo kuelekea visiwani Zanzibar ambayo itasaidia kwa kiwango kikubwa kufungua uchumi wa Wilaya hiyo kutokana na uwepo wa utalii wa mbuga ya Saadan. 

Pia uwepo wa boti hiyo unatajwa kwenda kurahisisha usafiri hususani kwa watu wanaotokea Mikoa ya Tanga,  Kilimanjaro, Arusha na Manyara badala ya kwenda kupanda jijini Daresalaam watakuwa wanapitia Pangani. 

Waziri Aweso ametoa ombi hilo mbele ya kikao cha Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah akiwa kwenye mkutano wake wa ndani na wanachama wa chama cha mapinduzi ccm Wilayani Pangani. 

Aweso amesema miongoni mwa mahitaji makubwa ya watu wa Pangani ni pamoja na upatikanaji wa boti hiyo ambayo uwepo wake utakwenda kuchochea kasi kubwa ya maendeleo kati ya Zanzibar,  Pangani na maeneo mengine. 

"Wilaya yetu ya Pangani Jigrafia yake inafanana na Zanzibar lakini pia wilaya yetu ya ya Pangani ina mbuga ya Saadan Zanzibar nyinyi utalii ni mkubwa lakini mbuga hakuna leo wilaya yetu ya Pangani kwanamna ilivyokaa ukienda huku kuna Mombasa,  Tanga mjini,  Muheza,  Handeni na Kilindi na Wilaya zingine lakini pia tuna Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha na Manyara leo mtu akitaka kwenda Zanzibar hadi aende Daresalaam, "

"Tukipata Fast boat hapa Pangani maana yake watalii wataweza mchana kuja Pangani jioni wakarudi zao Zanzibar hii itaifungua sana Pangani kiuchumi nataka niwaambie ndugu zetu hapa tunapoelekea ni suala tu la uchumi Rais wetu anatufanyia mambo makubwa sana sisi watu wa Pangani tuna deni kubwa la kumlipa Rais wetu,"alisisitiza Aweso. 

Akijibu changamoto ya Mbunge huyo,  Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah amesema wapo katika hatua za mwisho za mchakato wa manunuzi ya boti mpya mbili za kisasa zinazokwenda kwa kasi, zitakazofanya safari kati ya Tanga, Pemba, Unguja, Dar es Salaam na Mombasa nchini Kenya.

Makamu wa Rais Abdulla amesema, uundwaji wa boti hizo utakamilika miezi mitatu ijayo, na zitafungua njia zaidi za uchumi kati ya Zanzibar na maeneo zitakapokwenda ikiwemo Tanga. 

Amesema, baada ya kuwasili na kuanza safari kwa boti hizo, atashirikisha azma ya kuwepo safari za kupitia Pangani kama ilivyowasilishwa na Mhe Aweso kuwa ni miongoni mwa mahitaji ya wakazi wa wilaya hiyo

"Nataka niwaambie uundwaji wa boti hizo utakamilika miezi mitatu ijayo, na zitafungua njia zaidi za uchumi kati ya Zanzibar na maeneo zitakapokwenda ikiwemo Tanga naaeneo mengine, "alisisitiza Abdullah. 

Katika Kikao hicho Mwenyekiti wa ccm Mkoa Tanga Rajab Abrahaman Abdallah amesema watahakikisha wanaendelea kukijenga chama katika Mkoa wa Tanga ili ifikapo uchaguzi chama hicho kishinde kwa kishindo. 

Rajab amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akipeleka miradi mikubwa ya kimaendeleo katika Mkoa wa Tanga hususani katika sekta ya Afya,  elimu,  barabara,  maji na umeme. 

"Sisi kwenye Mkoa wa Tanga tuna vijijo 779 mheshimiwa Rais amekwishapeleka umeme kwenye vijiji vyote 779 kwenye Mkoa Tanga hata hapa Pangani tuna umeme kwenye vijiji vyote 33, lakini Handeni,  Lushoto,  Mkinga,  Muheza na Kilindi pia tuna umeme mheshimiwa Rais ameshapeleka umeme katika maeneo yote hayo, "alibainisha Rajab. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post