Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, akitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Agosti 29,2024.
Na
Mapuli Kitina Misalaba
Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson
Mnyawami, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameeleza kuwa matukio ya
hivi karibuni yameibua wasiwasi miongoni mwa wananchi, hususan baada ya tukio
la kijana Meshack Paka (20) kupoteza maisha na wengine wanne kujeruhiwa.
Aidha, raia wapatao 134 wanashikiliwa na Jeshi la
Polisi, huku kukiwa na malalamiko ya kukosa huduma muhimu kama dhamana na
matibabu.
CHADEMA imehimiza Jeshi la Polisi kujenga mahusiano
mazuri na wananchi ili kuhakikisha usalama na kuzuia ghasia, ambapo Mnyawami
ametoa wito kwa vyombo vya usalama kushughulikia kwa umakini matatizo yanayozua
taharuki katika jamii, ili kudumisha amani na utulivu.
Pia, chama hicho kinaitaka serikali kuwaachilia huru
raia waliokamatwa, na kuchunguza kwa kina chanzo cha matukio haya ili hatua
stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.
Katika tukio lingine, CHADEMA imeomba Jeshi la
Polisi kuchunguza tukio la kijana Baraka Njile Makongolo ambaye alifariki dunia
baada ya kudaiwa kushambuliwa akiwa mikononi mwa askari pia Chama hicho
kimesisitiza umuhimu wa kuhakikisha haki inatendeka na kuwajibika kwa mujibu wa
sheria.
CHADEMA pia imewapongeza wananchi wa Jimbo la
Itilima kwa kujitolea kulinda usalama wao, na imetoa wito kwa wananchi wengine
kuchukua tahadhari kwa ushirikiano na vyombo vya usalama.
CHADEMA Kanda ya Serengeti imetoa wito kwa pande
zote zinazohusika kuhakikisha usalama na haki za wananchi zinaheshimiwa.
Mnyawami amesema, “Tunasisitiza ushirikiano kati ya vyombo vya usalama na
wananchi ili kudumisha amani na utulivu katika jamii zetu.”
Kanda ya Serengeti inajumuisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.
Social Plugin