Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PEPFAR YAPONGEZA UTEKELEZAJI WA AFUA ZA KUPAMBANA NA UKIMWI MKOANI TANGA


Na Hadija Bagasha Tanga 

Utafiti wa hivi karibuni wa Athari za VVU Tanzania 2022-2023 (Tanzania HIV Impact Survey 2022-2023) umeonesha kuwa jitihada mbalimbali za Serikali pamoja na wadau wa afya mkoani Tanga zimefanikisha wapokea huduma za VVU kufubaza virusi kwa asilimia 93.5.

Serikali kupitia timu za mkoa na halmashauri (R/CHMT) kwa kushirikiana na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS), kupitia mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), kupitia kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa cha Marekani (U.S. CDC) wamekuwa mstali wa mbele katika kutoa huduma za kinga, matunzo na tiba kwa watu walio kwenye hatali ya kupata maambukizi au ambao wanaishi na maambukizi ya VVU.

Pamoja na mambo mengine, Shirika la THPS limekuwa likishiriki katika utekelezaji wa afua zinazolenga kutoa kuduma rafiki za VVU kwa vijana, kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, na kuhakikisha wapokea huduma wanabaki kwenye huduma na kufubaza VVU.

Hayo yalibainishwa wakati wa ziara ya waandishi wa habari mkoani Tanga walipotembelea hospitali ya wilaya ya Korogwe (Magunga ), Kituo cha Afya St.Raphael pamoja na kituo cha afya cha Mombo vinavyowezeshwa na Shirika la THPS.

Kaimu Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI (RACC) mkoani Tanga, Bi. Judith Kazimoto, alisema THPS kupitia mradi wa Afya Hatua, kwakushirikiana na timu za usimamizi wa Afya za Mkoa na Wilaya, wanatekeleza afua mbalimbali za kupambana na VVU, katika vituo 67 vya afya vilivyopo mkoani humo, ikiwemo hospitali ya mji wa Korogwe.

“Kuanzia Oktoba 2023 hadi Julai 2024, Kliniki ya tiba na matunzo ya VVU ya Hospitali ya Mji wa Korogwe ilikuwa na jumla ya vijana 134 wenye umri wa miaka 15 hadi 25 ambao walikuwa wameandikishwa katika huduma za VVU na asilimia 90% ya vijana hao walikuwa wamefubaza makali ya VVU”, alisema Bi. Kazimoto.

Ili kuhakikisha huduma bora za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kina mama wajawazito wanaoishi na VVU hupatiwa huduma zote muhimu, na mara baada ya kujifungua, watoto wao husajiliwa na kuchukuliwa vipimo vya VVU mapema.


Kupitia mradi wa Afya Hatua, watoa huduma katika kituo cha Afya cha St. Raphael huhakikisha usajili wa Watoto hao unafanyika na wanachukuliwa sampuli za damu ili kufanyiwa kipimo cha VVU ndani ya wiki sita baada ya kuzaliwa kwao na kuhakikisha wanapatiwa huduma stahiki.

“Kwa kipindi cha kuanzia Oktoba 2023 hadi Julai 2024, jumla ya wapokea huduma za VVU wajawazito 26 walijifungua katika kituo hicho. Watoto waliozaliwa na kina mama hawa walisajiliwa ndani ya siku saba baada ya kujifungua. Kati ya hao, 24 (93%) walichukuliwa vipimo na wote (100%) na matokeo yalionesha wote walizaliwa bila maambukizi ya VVU”, alisema Bi. Kazimoto.


Mradi wa Afya Hatua kwa kushirikiana na watoa huduma za afya katika kituo cha afya cha Mombo, wilayani Korogwe, wamehakikisha ufuasi sahihi na kubaki katika huduma za dawa za kufubaza makali ya VVU miongoni mwa wapokea huduma katika kituo hicho na hivyo kupelekea asilimia 99% ya wapokea huduma 1,501 waliosajiliwa katika kituo hicho kuwa wamefubaza VVU.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari waliofika katika kituo cha afya cha Mombo, mmoja wa wapokea huduma ambaye pia ni mwelimishaji rika, Silvia Somi amesema kutokana na huduma anayopatiwa na kufata masharti anayopewa na wataalam wa afya anaendelea na afya njema na anaendelea kuhamasisha wapokea huduma wenzake kubaki kwenye huduma.

"Wengi wanakuja wakiwa wameshakata tamaa na hawaelewi pa kuanzia lakini kutokana na shuhuda ambazo tumekuwa tukiwapatia watu wameendelea kuwa na sisi wengi wamebaki kwenye huduma tunawatafuta wengine majumbani na kuhakikisha wanaendelea na huduma ya dawa”, alisema Silvia.

Awali, Mratibu wa PEPFAR nchini Tanzania, Bi. Jessica Greene alisema katika kipindi cha miaka 21 iliyopita, Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR imewekeza zaidi ya Dola Bilioni 7 nchini Tanzania kukabiliana na janga la VVU.

“Wakati PEPFAR ilipoanza kazi nchini mwaka 2003 kulikuwa na watu takriban 1,000 waliokuwa kwenye matibabu, lakini kwa sasa tunasaidia watu zaidi ya Milioni 1.5 waliopo kwenye huduma ya tiba na matunzo, na vifo vinavyotokana na UKIMWI nchini Tanzania vimepungua kwa asilimia 76 tangu mwaka 2023 na maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 58”, alisema Bi. Greene.


Bi. Greene alisema lengo ni kukomesha VVU/UKIMWI kama tishio kwa Afya ya Umma ifikapo mwaka 2030 ni kubwa lakini linaweza kufanikiwa huku akieleza Serikali ya Marekani inavyojivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania kufikia malengo ya UNAIDS 95-95-95 ifikapo mwaka 2025.

“Malengo hayo yanalenga asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU kufahamu hali zao, asilimia 95 ya waliogundulika kuwa na VVU wapate matibabu na asilimia 95 ya wale walio kwenye matibabu waweze kufubaza VVU”, alisema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com