TAKUKURU KAGERA YAFUATILIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO 20 YA BILIONI NNE


Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kagera akizungumza na waandishi wa habari 

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Mkoani Kagera imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi Cha Aprili hadi Juni 2024 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni nne.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi ya Takukuru Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera Julai 6,2024, Naibu Mkuu wa Takukuru Kagera Bw. Ezekia Sinkala amesema kuwa miradi iliyofuatiliwa ni ya ujenzi wa miundombinu ya maji, zahanati, barabara, ujenzi wa shule mpya moja na ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari ikiwa inalenga kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa inaendana na thamani ya fedha iliyotumika.


Aidha Bw. Sinkala amesema kuwa katika miradi hiyo 20 wamebaini miradi 18 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.8 kuwa na mapungufu yaliyohitaji marekebisho sawa na asilimia 90 ya miradi iliyofatiliwa ambapo mapungufu hayo ni pamoja na vifaa vya ujenzi kutokuwa bora na kiwango ambacho kinatakiwa, mapokezi ya vifaa vya ujenzi bila kurekodiwa kwenye leja, utaratibu wa mapokezi ya vifaa unaotia shaka pamoja na uandaaji wa mihtasari ya kamati mbalimbali unaotia shaka.

Aidha amewataka wasimamizi wa miradi kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi husika pia kufanya marekebisho ya mapungufu katika miradi iliyobainika kuwa na mapungufu kwa wakati.

Sambamba na hayo amesema kuwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2024 wamepokea malalamiko 132 na kati ya malalamiko hayo, malalamiko 48 hayahusu Rushwa hivyo walalamikaji walielimishwa, huku malalamiko 84 yalihusu rushwa na kufunguliwa majalada ya uchunguzi na kati ya majalada hayo 84, uchunguzi wa majalada 11 umekamilika na hatua mbalimbali za kisheria zinatarajia kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa huku majalada 73 uchunguzi bado unaendelea.


Ameongeza kuwa katika sekta ambazo zinalalamikiwa kutokana na taarifa 132 ni Uvuvi, Ardhi, Elimu, Afya, Nishati pamoja na sekta binafsi huku akisema kuwa malalamiko ya rushwa yamekuwa mengi kutokana na kuongezeka kwa malalamiko ya madai baina ya wananchi na kwamba kwa upande wa mashtaka mashauri mapya 14 yamefunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya mashauri 38 yanayoendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali Mkoani Kagera na katika kipindi hicho mashauri 12 Jamhuri imeshinda.


Hali kadhalika Bw. Sinkala amesema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024 Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa imeweka malengo ya kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2024 ambavyo ni kuimarisha ushirikiano na wadau ili kuihamasisha jamii kuzuia vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa,


Pia kuendelea kuelimisha makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi, vyama vya siasa na wasimamizi wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika bila kuwepo vitendo vya rushwa, kuwashirikisha wananchi na wadau wa uchaguzi ili watoe taarifa za vitendo vya rushwa katika chaguzi pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote watakao jihusisha na vitendo vya rushwa na uvunjifu wa sheria, kanuni na miongozo inayoongoza uchaguzi wa Serikali za Mitaa.


Ametoa wito kwa wananchi wenye sifa kutumia haki yao kikatiba kujiandikisha na kupiga kura lakini pia kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa, huku akiwatahadhalisha wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutojihusisha na vitendo vya rushwa na kwamba Takukuru Mkoa wa Kagera watawachukulia hatua za kisheria dhidi ya wale wote watakao jihusisha na vitendo vya rushwa kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post