Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MHE. SIMBACHAWENE: TUTAZUIA WATUMISHI KUINGIA OFISINI NA SIMU ZA MKONONI


Na. Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ametoa rai kwa Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE Tanzania kuhamasisha Watumishi wa Umma katika sehemu zao za kazi kujituma na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo wakati akifunga semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE iliyofanyika kuanzia tarehe 26 hadi 29 Agosti, 2024 katika Hoteli ya Lushgarden jijini Arusha.

Katika hotuba yake alisitiza Waajiri na Viongozi hao kutafuta namna bora na kuishauri Serikali ili kuweka utaratibu wa kuzuia watumishi wa umma kuingia kazini na simu zao za mkononi kwa kuwa zimekuwa kikwazo kwa utoaji wa huduma bora kwa umma.

“Nchi nyingine watumishi hawatumii simu wakiwa ofisini, kazi yao ni kutoa huduma kwa umma, lakini sisi tunachati tu badala ya kufanya kazi.
 Piteni kwenye ofisi mbalimbali za umma muone watumishi walivyobize na matumizi ya simu zao za mkononi tangu wanapoingia kazini, mathalani mtumishi ana magrupu ya ‘WhatsApp’ zaidi ya ishirini na anasoma yote na kujibu, hivyo kutumia muda wa mwajiri kwa manufaa binafsi. Ninawasihi muingilie kati na kuishi kaulimbiu yenu ya Huduma Bora, Maslahi zaidi”.

Aliongeza kuwa, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mkuu wa Utumishi wa Umma anafanya jitihada kubwa za kuboresha masilahi ya watumishi ikiwa ni pamoja na kuelekeza kufanya maboresho ya kikokotoo, kupandisha madaraja na mishahara, kulipa malimbikizo na kutoa ajira mpya kwa lengo la kuboresha utumishi wa umma.

Aidha, alibainisha kuwa wajibu wa msingi kwa mtumishi wa umma ni kuwahudumia wananchi wakati wote ili waweze kufanya shughuli zao za kujenga taifa kwa urahisi, lakini watumishi wamekuwa hawawajibiki ipasavyo na hivyo kuathiri mnyororo wa kuwatumikia wananchi.

Awali, Mwenyekiti wa TUGHE Taifa Bw. Joel Kaminyoge amesema wameamua kuwakutanisha waajiri na viongozi wa TUGHE kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya chama na waajiri na zaidi kubainisha changomoto katika utumishi wa umma na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

Bw. Kaminyoge amempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa msikivu wakati wote wanapowasilisha shida zao na kuzitafutia ufumbuzi haraka. Hivyo, yeye na viongozi wenzake waliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika utumishi wa umma.

Halikadhalika, Katibu wa Mkuu wa TUGHE Taifa Bw. Hery Mkunda aliongeza kwa kumshukuru Mhe. Simbachawene kwa kutenga muda na kuitikia wito wa kuwa mgeni rasmi wakati wa kufunga semina hiyo ambayo wamepata kujifunza masuala mbalimbali yenye manufaa kwa washiriki na taifa kwa jumla.

Bw. Mkunda, amewapongeza waajiri wote walioruhusu watumishi wao kushiriki semina hiyo na amesema hawatajuta kuwaruhusu viongozi hao kwa kuwa wameongezeka thamani kutokana na elimu iliyotolewa katika semina hiyo.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com