BUNGE LAPITISHA MUSWADA, MAREKEBISHO YA SHERIA ZA ULINZI WA MTOTO



Na WMJJWM, Dodoma

Bunge la Tanzania limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria zinazohusu ulinzi wa mtoto wa mwaka 2024 leo Agosti 30, 2024 jijini Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, akiwasilisha Muswada huo amesema madhumuni yake yanalenga kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa utekelezaji wa baadhi ya masharti ya sheria hizo ili kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto.

Amebainisha kuwa, muswada huo umetoa mapendekezo katika sheria tatu ambazo ni Sheria ya Makosa ya Kimtandao Sura ya 443, Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 na Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21.

Waziri Dkt. Gwajima amesema kazi ya kuboresha sheria na miongozo mbalimbali inayohusu ulinzi wa mtoto itaendelea kufanyika kama kazi endelevu kwani, kwa sasa kasi ya mabadiliko kwenye jamii ni hasa katika mazingira ya maendeleo ya ulimwengu wa kidigitali.

"Kila mwaka hatutasita kuja na marekebisho ya Sheria kutokana na Kasi ya mabadiliko ya kijamii kwenye ulimwengu wa maendeleo ya kidigitali kwani, kasi hiyo pia inagusa maendeleo na ustawi wa maisha ya watoto wetu katika rika mbalimbali" amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Michael Kembaki ameishauri Serikali kuhakikisha sheria zote zinazohusu ulinzi wa mtoto zipitiwe upya ili kuendana na mazingira ya sasa, kutenga bajeti ya kuendesha mabaraza ya watoto pamoja na kuongeza kasi ya kuajiri Maafisa Ustawi wa Jamii.

Nao baadhi ya wabunge wakichangia kuhusu Muswada huo wameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kufanya marekebisho ya Sheria zinazuhusu ulinzi wa mtoto ili kumlinda mtoto na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na vitendo vya ukatili na udhalilishaji.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post