Katika jitihada za kuongeza uelewa wa umuhimu wa huduma za Maji na utunzaji wa vyanzo vya maji Nchin kuanzia ngazi ya jamii, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetembelea Shule ya Msingi Kibasila, Iliyopo Wilaya ya Kisarawe na kufungua klabu ya mazingira kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi kuhusu kutunza mazingira na kulinda miundombinu ya majisafi.
Ndugu Hashura Kamugisha, Afisa Mawasiliano amesema dhumuni la kuanzisha klabu za mazingira katika ngazi ya shule za Msingi na Sekondari ni kutengeneza kizazi bora kinachofahamu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na namna bora ya kutunza vyanzo vya maji ili kuweza kuwa na huduma ya maji endelevu huku maji yakiwa ni sehemu muhimu katika maisha yao.
“Maji tunayotumia katika shughuli zetu za kila siku yanapatikana kwenye mazingira yetu kupitia vyanzo mbalimbali hivo ni jukumu letu sote kutunza vyanzo hivyo kwani tukitunza mazingira nasi yatatutunza" amesema Ndugu Hashura.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Mwalimu Godfrey Haule ambae ni mlezi wa klabu ya Mazingira shuleni hapo ameishukuru DAWASA kwa jitihada za kufikia watoto wa shule za msingi na kutoa elimu ya maji na usafi wa Mazingira akiamini itakuwa chachu ya mabadiliko kwa vijana hao.
“Elimu ya maji na usafi wa Mazingira ni elimu inayorithi kizazi na kizazi kwakuwa inalenga mabadiliko ya kitabia hivyo tunaishukuru sana DAWASA kwa jitihada za kutoa elimu hiyo kwa vijana wetu hakika ni adhina ya kudumu” amesema Mwl. Haule.
Ndugu. Yonna Abdallahi, mwanafunzi na mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa mazingira ya shule ya msingi Kibasila ameishukuru Mamlaka kwa kuwa mlezi na kutoa nafasi ya wao kujifunza mambo mbalimbali ya Maji na Usafi wa Mazingira na kuomba nafasi ya kuendelea kujifunza kwa vitendo ili kufahamu zaidi namna Mamlaka inavyoendesha shughuli zake.
Social Plugin