Chamwino-Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha ardhi inayotengwa kwaajili ya kilimo cha zabibu inalindwa ili usifanyike ujenzi wa makazi katika ardhi hiyo.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Kiwanda cha Kusindika Zabibu kilichopo Chinangali II Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani humo. Amesema kasi ya ujenzi wa makazi imekuwa kubwa mkoani Dodoma hivyo ni vema wataalamu wa mipango miji na wapimaji viwanja kuzingatia maeneo ya kilimo cha zabibu kubaki kama yalivyopangwa.
Aidha amewasihi wananchi wa mkoa wa Dodoma kuongeza jitihada katika kulima zabibu ili kiwanda hicho kiwe na manufaa zaidi.
Amesema Tanzania hutumia takriban shilingi Bilioni 19.5 kila mwaka kuagiza wastani wa lita milioni 10 za mchuzi wa zabibu nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya ndani hivyo uwepo wa kiwanda hicho unatatua changamoto nyingi za usindikaji na uhifadhi wa zabibu pamoja na kuzuia upotevu kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya kuongezea thamani na uhifadhi.
Ameongeza kwamba Viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ikiwemo zabibu kwa ajili ya matumizi yetu ya ndani na kuuza ziada nje ya nchi ni miongoni mwa vipaumbele muhimu katika agenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya 10/30 – yaani kufikia ukuaji wa asilimia 10 katika Sekta ya Kilimo ifikapo 2030.
Makamu wa Rais amesema Serikali imeliingiza zao la zabibu katika orodha ya mazao ya kimkakati ambayo ni ya kipaumbele katika kuendelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi. Amemuagiza Waziri wa Kilimo kuhakikisha upatikanaji wa miche bora kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Halmashauri za wilaya husika, pamoja na kuimarisha huduma za ugani za zao la zabibu.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma kuepukana na uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto na kukata miti ovyo. Amewataka kuzingatia wajibu wa kutunza vyanzo vya maji na ardhi oevu ili kuunusuru mkoa huo na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Chamwino kujitokeza katika kutoa maoni katika mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa 2050 pamoja kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Awali Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kiwanda hicho ni matokeo ya kilio cha wakulima wa zabibu mkoani Dodoma kukosa sehemu ya kupeleka zao hilo na hivyo kupelekea kupata hasara mara kwa mara. Ameongeza kwamba kwa sasa hatua ya pili ya ujenzi wa kiwanda hicho ni kuwajengea matenki wakulima wa zabibu ili waweze kuzalisha na kuwa na uwezo wa kuchagua kuuza zabibu kama tunda au kuuza kama mchuzi baada ya kuchakata.
Amesema kutokana na Mkoa wa Dodoma kuwa na upotevu mkubwa wa maji, tayari Wizara ya Kilimo ina miradi ya umwagiliaji ikiwemo ujenzi wa bwawa la kukusanya maji Wilaya ya Chamwino pamoja na mradi wa hekari 11,000 wa kilimo cha umwagiliaji katika Jimbo la Mtera.
Kiwanda cha Kusindika Zabibu kinagharimu shilingi bilioni 2.1 na kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchakata tani 300 kwa mwaka na kuhifadhi lita 220,000za mchuzi wa zabibu kwa mwaka. Kiwanda hicho kitahudumia wakulima takribani 120 kutoka katika maeneo ya karibu na kiwanda ikiwemo shamba la zabibu la BBT Chinangali.