DKT. MPANGO AAGIZA UJENZI WA BARABARA KUZINGATIA WATEMBEA KWA MIGUU NA BAISKELI



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameagiza Wizara ya Ujenzi kufanya maboresho katika ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini kwa kuhakikisha wanaongeza njia za waenda kwa miguu, waendesha pikipiki na baiskeli ili kupunguza ajali za barabarani.



Agizo hilo amelitoa leo Agosti 26, 2024, wakati akikagua banda la Wizara ya Ujenzi jijiji Dodoma katika ufunguzi wa “Wiki ya nenda kwa usalama barabarani” nchini inayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Taifa la Usalama barabarani ikiongozwa na kauli mbiu ‘Endesha Salama, Ufike Salama’.


Dkt. Mpango amesisitiza kutokucheleweshwa kwa uwekaji wa mawe ya mipaka ya barabara katika hifadhi za barabara kwa miradi inayojengwa ili kuilinda na kuzuia uvamizi wa barabara hizo.


“Muangalie usanifu wenu na kuhakikisha barabara zote zinakuwa na njia za watembea kwa miguu hasa mijini, pia njia za waendesha baiskeli na pikipiki”, hakikisheni hili mnalisimamia”, ameelekeza Makamu wa Rais.


Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amelitaka Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kuhakikisha wanasimamia ukaguzi makini wa vyombo vya moto mwaka mzima na sio kusubiri kipindi cha wiki ya Nenda kwa Usalama. 




Aidha, Dkt. Mpango ameeleza kuwa ili kupunguza ajali za barabarani zinazosababishwa na Makosa ya Kibinaadamu ni vyema madereva kuongeza umakini na kudhibiti vihatarishi vya ajali barabarani kwani takwimu zinaonesha kwa mwaka 2023 ajali zilikuwa 1,733 vifo 1,647 na majeruhi 2.716. 



Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhandisi Hamadi Masauni amesema uwepo wa matumizi ya mifumo ya TEHAMA barabarani ikiwemo Kamera sio tu inapunguza ajali bali inapunguza pia ukiukwaji wa maadili kwa baadhi ya Askari ikiwemo masuala ya Rushwa. 



Naye, Mwenyekiti wa Baraza La Taifa la Usalama Barabarani na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema katika jitihada za Kupambana na Makosa ya kibinadamu yanayosababisha ajali barabarani Baraza hilo katika kusherehekea miaka 50 yake, limekuja na mkakati maalumu ikiwa na maeneo kumi na Moja ya kuzingatiwa ikiwemo kudhibiti madereva walevi barabarani.


Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi, Mhandisi, Kashinde Musa amesema katika bajeti ya mwaka 2024/2025 Wizara ya Ujenzi imetenga bajeti kwa ajili ya kupunguza msongamano katika majiji matano na kusisitiza kuwa usanifu ambao utafanywa utazingatia watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na pikipiki.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post