Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amelitaka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kufanya ukaguzi makini na endelevu wa vyombo vya moto mara mbili kwa mwaka pamoja na kudhibiti magari yanayobeba wanafunzi Mashuleni kwani baadhi ya magari hayo yamekuwa na hali mbaya inayotishia usalama wa Wanafunzi pamoja na madereva wao
Dkt. Mpango ameyasema hayo katika Viwanja vya Jamhuri Jijini Dodoma leo Agosti 26, 2024 wakati akifungua Maadhimisho Wiki ya Nenda kwa Usalama Barababani ambayo Kitaifa yamezinduliwa Dodoma huku akisisitiza kuwa yapo magari yanayobeba wanafunzi kuliko uwezo wake na baadhi ya madereva kuonekana kukosa uweledi na uadilifu jambo linalosababisha madhara mbalimbali ikiwemo ajali.
" Nina mfano halisi ile ajali ya hovyo kabisa iliyotokea Mkoani Arusha na kusababisha Watanzania kuondokewa na watoto wetu Saba.
“Ninawataka Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama Barabarani mkasimamie na muhakikishe kwamba dereva anayepata Leseni ni yule aliyepitia mafunzo stahiki na umahiri wa uendeshaji wa vyombo vya moto, na hii inajumuisha Madereva wote wa magari ya abiria, mizigo, bodaboda na Bajaji.” Amesema
Aidha, Mheshimiwa Dkt. Mpango amepongeza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi huku akisisitiza kutoa nafasi kwa madereva Wanawake kwani mara kadhaa wanaonekana kuwa makini zaidi ikilinganishwa na baadhi ya wanaume.
Awali Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Wizara hiyo itaendelea kusimamia Jeshi la Polisi pamoja na kutoa ushirikiano kwa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kwa kutumia teknolojia ya kisasa ikiwa ni pamoja na kufunga kamera barabarani ili kusaidia kupunguza ajali barabarani, kupata upelelezi wa uhakika na wa haraka ikiwemo kubaini mapungufu pale ambapo kuna kosa limefanyika.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhe. Daniel Sillo amesema pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka 50 ya Usalama Barabarani hali ya Usalama Barabarani imeimarika na kuwa yenye tija ambapo Baraza la Taifa la Usalama Barabarani limeweza kujenga majengo ya Ofisi Sita za Makatibu wa Mikoa ikiwa ni pamoja na kununua magari ya doria 31 kwa kushirikiana na wadau wa Usalama wa Barabarani
Amesema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto kwa kutumia Mitambo ya kisasa
"Katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Arusha mwaka 2021 kuhusiana na ushirikishwaji wa wadau katika ukaguzi wa vyombo vya moto kwa Teknolojia ya kisasa Jeshi la Polisi na Baraza la Taifa la Usalama Barabarani tuliingia ubia na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kutumia mitambo ya kisasa ya ukaguzi wa vyombo vya moto kwa kuzingatia sheria ya PPP. Alisema Sillo
Aidha Mhe. Sillo alihitimisha kwa kusema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuepusha ajali barabarani, bado kuna tatizo la baadhi ya madereva wa magari na pikipiki kutokufuata sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali, alitoa Pole kwa watu wote waliopoteza wapendwa wao pamoja na waliopata vilema vya maisha kutokana na ajali za barabarani.