MKAGUZI Mkuu wa Mafuta kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati, Arthur Lyatuu, akizungumza kwenye banda la EWURA katika maonesho ya wakulima Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni,jijini Dodoma .
Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahamasisha wafanyabiashara wa mafuta kuwekeza vituo vya bidhaa hiyo maeneo ya vijijini kwa kuwa imerahisisha masharti ya ujenzi wa vituo hivyo hali itakayosaidia kukomesha uuzaji holela wa bidhaa hiyo kwenye vidumu na maeneo yasiyo rasmi unaweza kusababisha milipuko na kusababisha maafa hivyo kuweza kukidhi viwango vya usalama, utunzaji wa mazingira, mali na watu.
Mkaguzi Mkuu wa mafuta, EWURA Kanda ya Kati, Arthur Lyatuu, alisema hayo kwenye maonesho ya wakulima yanayofanyika viwanja vya Nzuguni, Dodoma .
"Tunajitahidi kuhamasisha watu wajenge vituo vya mafuta ili kuimarisha huduma hii kule vijijini kwasababu maeneo hayo bado yba vituo vituo vichache na uhitaji wa bidhaa za mafuta umeendelea kuongezeka, hivyo vituo hivi vitasaidia kuondoa hatari iliyopo sasa ya watu kufanya biashara hiyo kwa kificho na maeneo hatarishi" alisema.
Lyatuu ameeleza zaidi kuwa, wapo wananchi wanaofanya biashara hiyo kiholela na EWURA inapowabaini imekuwa ikiwashauri kufungua kituo kidogo cha mafuta ili kufanya biashara hiyo kwa njia salama kuliko kuweka kwenye madumu makubwa ambayo yanaweza kuleta mlipuko kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara makubwa ikiwamo vifo na uharibifu wa mali huku ikiwa pia ni kinyume cha sheria. Lyatuu, alisema mafuta yanapokuwa kwenye matenki ya chini ya ardhi siyo rahisi kulipuka kwakuwa yanakuwa salama sana.
Kadhalika alisema ili kuhamasisha uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini EWURA, imelegeza masharti ili kuongeza wigo wa huduma.
"Mtu ambaye anataka kuwekeza kituo cha mafuta kijijini Mamlaka imelegeza masharti ambapo maombi ya kibali cha ujenzi wa kituo kijijini ni shilingi 50,000 tu, gharama za maombi ya leseni pia shilingi 50,000/ na leseni shilingi 100,000/ inayolipwa mara moja kwa miaka mitano ambapo awali ilikuwa gharama sawa kwa maeneo yote",alisema
Vile vile, alisema masharti ya tathmini ya usalama wa mazingira ya eneo la ujenzi wa kituo cha mafuta kijijini ni tofauti na ilivyo mjini. Mjini lazima Baraza la usimamizi wa mazingira (NEMC) wafanye tathmini lakini kijijini ukaguzi unafanywa na halmashauri husika na muombaji kuandikiwa barua na Mkurugenzi wa halmashauri.