Na Mariam Kagenda _Kagera
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera imevuka lengo la makusanyo ya mapato ya ndani kwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 8.6 sawa na asilimia 125 ya lengo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe.Magongo Justus amesema hayo kwenye kikao cha baraza la Madiwani cha kujadili taarifa za robo ya nne ambacho kimefanyika Agosti 16 mwaka huu katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba
Mhe.Magongo amesema kuwa awali walikuwa wamelenga kukusanya shilingi bilioni 6.5 hivyo kutokana na ushirikiano wa Madiwani na watumishi wa Wilaya wameweza kuvuka lengo na fedha hizo zimeenda kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Tulipanga kukusanya na kutumia Bilion 6.5 lakini tumefanikiwa kukusanya bilioni 8.6 ambayo ni sawa na asilimia 125 jambo ambalo limepelekea kutekeleza miradi mbalimbali katika ngazi zetu za kata na vijiji lakini pia kuindesha halmashauri yetu"
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga amelitaka baraza la madiwani kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Pia amewataka madiwani kusimamia swala la lishe mashuleni ili kuondoa hali ya udumavu kwa watoto ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya lishe kwa wazazi na walezi.
"watoto wetu huko wanasoma kuanzia asubuhi mpaka jioni hawajapata chakula jambo hili lazima tulikatae sote na tuseme watoto wetu, wazazi wetu huko wachangie chakula kwa watoto wetu ili wasome katika mazingira rafiki"
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, wakuu wa taasisi, Kamati ya usalama ya wilaya na viongozi wa dini.
Social Plugin