NA MWANDISHI WETU
Katika kuelekea zoezi la Uboreshaji wa Daftari la mpiga kura, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama Mkoani Shinyanga imekutana na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Huheso katika kujadili namna Bora ya uhamasishaji wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo linalotarajia kuanza hivi karibuni.
Kikao hicho kimefanyika Agosti 7, 2024 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, huku zoezi hilo likitarajia kushika hatamu kuanzia Agosti 21 mpaka 27 mwaka, huku kukiwa na Vituo 249 vya uandikishaji katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu ambae pia ni Afisa Muandikishaji Mkuu katika zoezi Hilo Bi Khadija Mohamed Kabojela amewaomba wadau wote waliojitokeza kuwa mabalozi Wazuri katika kuihamasisha Jamii kuona umuhimu wa kushiriki Zoezi Hilo la kuboresha taarifa zao , sambamba na kujiandikisha upya kwa wale wenye sifa.
Bi Khadija amesema wadau ni chachu ya maendeleo hivyo Wana wajibu wa kushiriki zoezi la uhamasishaji wa Uboreshaji wa Daftari la mpiga kura kwa kutoa taarifa na Elimu sahihi juu ya umuhimu huo wa kujiandikisha kwani kwa kufanya hivyo kutamsaidia raia kutimiza haki yake ya msingi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kwa kupiga kura kwa Kiongozi anayemtaka.
Kwa Upande wake Afisa Uchaguzi Halmashauri ya Ushetu Bw. ELISHA MAHUNGO ametaja wenye sifa za kushiriki katika Zoezi Hilo la Uboreshaji wa Daftari la mpiga kura ni pamoja na Wapiga Kura wapya ambao hawajawahi kujiandikisha lakini Wana sifa za kupiga kura kuanzia miaka 18 na kuendelea, wale wote watakaotimiza miaka 18 ifikapo Oktoba kipindi Cha uchaguzi Mkuu mwaka 2025, lakini pia wale waliohamia kwa makazi ya kuishi katika Halmashauri hiyo, waliopoteza kadi zao, sambamba na kufuta taarifa za wapiga kura waliokosa sifa za kuendelea kuwepo katika daftari Hilo hasa waliotangulia mbele za haki.
Sambamba na Hilo alisema zoezi Hilo halitawahusu wananchi walio na vitambulisho visivyohitaji maboresho, hivyo amewasihi kuendelea kuvitunza kwa umakini mkubwa.
Kikao hicho kimehudhuliwa na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Huheso lenye makao yake makuu Mjini Kahama na ofisi yake ndogo iliyopo Halmashauri ya Ushetu inayotekeleza mradi wa EpiC unaofadhiliwa na USAID na kuratibiwa na FHI360 unaojihusisha na Upimaji wa VVU, huku wadau wengine wakiwa ni Jeshi la Polisi Ushetu ,Viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya Siasa, wawakilishi wa vijana pamoja na Vikundi vya hamasa vinavyopatikana ndani ya Halmashauri ya Ushetu.
Social Plugin