Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa rai kwa wadau wote wa Sekta ya Michezo kutumia Marathon zinazofanyika kupeleka tabasamu kwa watu wenye uhitaji mbalimbali kwa kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii zikiwemo huduma za Afya.
Dkt. Biteko amebainisha hayo leo Agosti 18, 2024 wakati wa Kilele cha CRDB Bank International Marathon 2024 iliyofanyika katika viwanja vya The Green, OysterBay jijini Dar es Salaam.
Amesema fedha zinazopatikana kupitia Marathon zimekuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya Watanzania ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo imekuwa mnufaika kwa watoto zaidi ya 400 kupata Masada wa matibabu ya magonjwa ya moyo katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
"Nichukue fursa hii kuwapongeza sana Benki ya CRDB kupitia Taasisi yenu ya CRDB Bank Foundation kwa ubunifu huu mkubwa wa kuandaa CRDB Bank International Marathon na jinsi mnavyoiendesha kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali pamoja na washiriki mmoja mmoja na kupata matokeo makubwa mkidhihirisha msemo wa Kiswahili wa "Haba na haba hujaza kibaba," amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa, fedha zote zilizotolewa katika kipindi cha miaka 4 kwa ajili ya kufadhili programu hizo ni zaidi ya Bilioni 1.2 za Kitanzania. "Hakika ubunifu wa CRDB Bank International Marathon umekuwa na matokeo chanya na mchango mkubwa kwa Taifa letu hususani katika sekta ya afya," amesisitiza Dkt. Biteko.
Kuhusu michezo, amesema Serikali inatekeleza miradi kadhaa kuhakikisha vijana wengi nchini wanashiriki katika michezo kwa kutambua kuwa michezo sio tu burudani bali ni ajira.
"Sehemu ya mipango ambayo inatekelezwa ni pamoja na kuratibu na kuyaboresha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ili kuwaandaa vijana wetu kuanzia wakiwa shule za msingi na sekondari," ameongeza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema michezo kwa sasa ni ajira kwa vijana, biashara kubwa na inajenga uchumi katika nyanja zote. Amesema Serikali imetoa ushirikiano kwa wadau wa Sekta ya michezo ili kufanya vijana wengi kushiriki na kupata ajira kupitia michezo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Bank ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema CRDB Marathon imefanyika kwa msimu wa tano na kuwakutanisha washiriki zaidi ya 10000 kutoka mataifa mbalimbali. Aidha marathon hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kusaidia Sekta ya afya kupata vifaa tiba na wenye uhitaji kupatiwa matibabu.