MASHINDANO YA RIADHA TANGA CITY MARATHON 2024 YAJA KIVINGINE

Mwenyekiti wa Chama cha Riadhaa Mkoa wa Tanga Sophia Wakati akizungumza wakati wa mkutano huo na wanahabari kuhusu mbio za Tanga City Marathon 






Usajili 'Tanga Marathon' 2024 kufanyika kwa mtandao 'Online'.


# Hamasa yatolewa kwa Wadau kuongeza nguvu udhamini mbio hizo, ni ili kuweza kunufaika na fursa zilizopo katika kuweza kujikwamua kiuchumi.


Na Oscar Assenga,TANGA


MASHINDANO ya Riadha 'Tanga Marathon 2024' yamekuja kivingine huku Usajili kwa washiriki wake utafanyika kwa njia ya mtandao 'Online' kupitia marathon. imartgroup.co.tz

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Msemaji Kamati ya Mashindano hayo, Fatma Mbinga, katika taarifa yake aliyoitoa kwa Vyombo vya Habari huko katika Ukumbi wa Amboni kwenye Hoteli ya Tanga Beach Resort Jijini Tanga alisema, huu ni msimu wa nane (8) kwa mbio hizo kufanyika Jijini Tanga.

Mbinga alisema, kwa mwaka huu usajili wa kumwezesha mtu kushiriki Tanga Marathon utafanyika kupitia njia ya mtandao huku akibainisha kuwa wamekuja kivingine na zawadi ni zenye kuvutia kwa washindi mbio hizo.

"Tunataraji Mbio zitakuwa tarehe 22/09/2024 leo tunatangaza jezi yetu ambayo ni nzuri, Tshirt yetu hii ina nafasi kubwa ya kufanya udhamini"alisema Bi Mbinga huku akitanabaisha kwamba medali zitatolewa kuanzia washindi wa mbio za Kilomita 5,10 hadi 21.


Aidha amesema kwamba, kwa mwaka huu 'Tanga Marathon' imejipanga kurejesha fadhila kwa jamii kwa kusaidia uimarishaji miundombinu ya elimu hususani madawati.


Awali akizungumza Katibu wa Chama cha Mchezo wa Riadha Mkoa wa Tanga  Hassan Mwagomba alisema kwamba mbio za Tanga Marathon kwa mwaka huu zitakuwa zile za kihistoria ,akiwasihi washiriki wa ndani na nje kuja kushiriki ili kujifunza mambo mbalimbali yenye tija.

Alisema kwamba kufanyika kwa mbio hizo itakuwa fursa adhimu kwa wanaTanga hususani Wajasiriamali akiwataja mama lishe kuuza chakula na biashara nyjngine ili kuweza kujiingizia kipato.

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama  Cha Riadha Mkoa wa Tanga,  Sophia Wakati  alitoa wito kwa wadau kujitokeza kwa wingi kufadhili mchezo huo na mingine ya aina hiyo inayokuwa ikifanyika katika mkoa huo wa Tanga.

Wakati alisema kwamba kwa kufanya udhamini Chama cha riadha itatoa fursa kwao kujifunza mambo mbalimbali huku wakinufaika na fursa za uwekezaji zilizoandaliwa na Serikali yao katika mkoa huo uliopo pembezoni mwa Bahari ya Hindi.

Tayari Kampuni ya Bima ya Bumaco, iMart Group Ltd na Tanga Beach Resort zimejitokeza kudhamini mashindano ya Tanga Marathon Mwaka 2024.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post