MIAKA 60 YA HIFADHI YA TAIFA MIKUMI YAZAA MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA UTALII


Miaka 60 ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa Mikumi imeleta mafanikio makubwa katika Sekta ya Utalii nchini yakichangiwa na jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa leo Agosti 31,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) wakati wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa Mikumi mkoani Morogoro ambapo amesema kupitia filamu maarufu ya “Tanzania: The Royal Tour” pamoja na filamu ya “The Amazing TANZANIA”zimekuwa chachu ya kukuza utalii na kuongeza idadi ya wageni wa ndani na nje ya nchi.

“Kufuatia jitihada hizo za Rais Samia, katika mwaka wa fedha 2023/2024 idadi ya watalii wa kimataifa waliofika nchini imeongezeka kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,808,205 Mwaka 2023” amesisitiza Mhe. Chana na kuongeza kuwa upande wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, kwa mwaka 2023/2024 jumla ya watalii 138,844 wametembelea Hifadhi hiyo sawa na ongezeko la asilimia 198.48 kutoka watalii 46,517 waliotembelea hifadhi hiyo kwa mwaka 2020/2021.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa watalii kwa kuboresha miundombinu ya utalii ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendokasi (SGR), kuimarisha Shirika la Ndege nchini (ATCL) na ujenzi wa barabara kurahisisha watalii kufikia vivutio mbalimbali.
Katika kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, Serikali kupitia Mradi wa REGROW inaboresha uwanja wa ndege kuwa wa kisasa katika eneo la Kikoboga, ujenzi wa malango ya watalii eneo la Doma na Kikwaraza, ujenzi wa kituo cha kutoa taarifa kwa wageni (VIC), kambi za kupumzikia wageni (Picnic Sites), maeneo ya malazi (Cottages & Campsites) na kuunganisha Hifadhi ya Taifa Mikumi kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.

Amesema miradi hiyo itakapokamilika itawezesha kuongeza idadi ya watalii kwa kuwa ndege kubwa zaidi zitaweza kutua ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi ambapo kwa wakati mmoja wageni zaidi ya 140 wataweza kuhudumiwa kwa pamoja.

Pia, amesema Serikali imepanga kujenga lango la kupokelea watalii watakaokuja Mikumi kwa njia ya reli ya ya kisasa ya mwendokasi (SGR) kupitia kituo cha reli ya SGR kilichopo kwenye mji wa Kilosa. Ujenzi wa lango hili utaleta chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Wilaya Kilosa hususan kwa vijiji vya Myombo, Mbamba na Kilangali.

Naye, Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Kuji amesema kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ilikua ikishika nafasi ya 14 kati ya hifadhi 21 katika ukusanyaji wa mapato ambapo kwa sasa iinashika nafasi ya 6.

Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Augustine Massesa amesema kupitia utalii wa Hifadhi ya Taifa Mikumi uchumi wa jamii zinazozunguka eneo hilo umeongezeka, wameweza kushirikiana na jamii kuwapa fursa za ajira, elimu ya uhifadhi, miradi ya maendeleo pamoja na kushirikiana na Askari wa Vijiji (VGS) kukabiliana na changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu.

Hifadhi hii ni hifadhi kongwe ambayo ni Hifadhi ya Taifa ya tano kuanzishwa baada ya Hifadhi za Taifa za Serengeti (1951), Ziwa Manyara (1960), Arusha (1960) na Ruaha (1964). inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964 kwa Tangazo la Serikali Na 465.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post