Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo akitembelea eneo la Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda ulioko Engaruka wakati wa ziara yake ya kikazi katika kata ya Engaruka Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha ili kuona maendeleo ya mradi huo.
Waziri wa viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Suleimani Jafo, amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 14 kwa ajili ya kulipa fidia Wakazi wa Kata ya Engaruka wilayani Monduri Mkoani Arusha ili kupisha ujenzi wa Kiwanda cha magadi soda unaotarajiwa kuanza utekelezaji hivi karibuni.
Vilevile Waziri Jafo amewahakikishia wakazi wa eneo hilo kuwa, kila anayestahili kulipwa fidia atapewa haki yake na kuwaasa kuacha udanganyifu kwenye ulipwaji wa fidia kwa kuwa Serikali ilishafanya uhakiki wa majina kwa wale wote wanaostahili kulipwa.
Waziri Jafo ameyasema hayo alipotembelea Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda ulioko Engaruka Wilayani Monduli Mkoani Arusha unaotekelezwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa lengo la kujionea hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mradi huo ikiwa ni ni muendelezo wa ziara yake Mkoa wa Arusha.
Aidha, ameushauri uongozi wa Wilaya ya Monduli kupima maeneo yote yanayo zunguka Mradi huo ili kuwezesha ujenzi wa makazi viwanda na biashara mbalimbali kwa mpangilio unaovutia.
Vile vile amesema kuwa Seikali itaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu muhimu kama barabara, maji na umeme ili kurahisisha utekelezaji wa Mradi huo kwa urahisi ikiwemo ubebaji na ufungaji wa mitambo mbalimbali ya kiwanda hicho cha kichakata madini hayo muhimu ambayo ni wezeshi kwa viwanda vingi vya uzalishaji wa vioo, dawa na bidhaa mbalimbali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Festus Kiswaga akiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli Muhsin Kassim amesema wapo tayari kupokea mradi huo huku wakitoa rai kwa wananchi kuchangamikia fursa zitakazotokana na utekelezwaji wa Mradi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo, (NDC) Dkt Nicolaus Shombe amebainisha kuwa NDC kama mwekezaji kwa niaba ya Serikali tayari imekamilisha hatua mabalimbali za kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kufanya tafiti za kiasi na ubora wa magadi, upembuzi yakinifu, tathmini ya athari kwa mazingira, uthamini wa mali za wananchi watakaopisha mradi na usanifu wa ujenzi wa kiwanda hicho ambacho kitakapo kamilika kitakuwa na na uwezo wa kuzalisha kimiminika cha Magadi soda tani milion moja kwa Mwaka.
Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wa Engaruka Viongozi wa eneo hilo wakiwemo Diwani na Mtendaji wa Kata ya Engaruka pamoja na Wenyeviti wa Vijiji vya Engaruka juu, Engaruka chini, Irerendeni pamoja na Oldonyo Lengai wameonyeshwa kufurahishwa na hatua ya Serikali kuamua kutekeleza mradi huo utawakaowaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo akitembelea eneo la Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda ulioko Engaruka wakati wa ziara yake ya kikazi katika kata ya Engaruka Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha ili kuona maendeleo ya mradi huo.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jaf, akiangalia na kupokea maelezo ya Kisima cha maji yenye magadi soda katika Mradi wa Kimkakati wa Magadi soda Engaruka kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo, (NDC) Dkt Nicolaus Shombe wakati wa ziara yake alipotembelea Mradi huo Engaruka Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.
Waziri wa viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo, akizungumza na wananchi wa Engaruka juu, Engaruka chini, Irerendeni pamoja na Oldonyo Lengai wanahusika na Mradi wa Magadi Soda, wakati wa ziara kutembelea Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda-Engaruka kwa lengo la kuona hatua mbalimbali za utekelezaji wake.