MRADI WA MILIONI 200 WARUDISHA TABASAMU KWEMBE, MALAMBA MAWILI NA KINGAZI

 


Adha ya upatikanaji wa huduma ya Majisafi na salama kwa wakazi takribani 10,000 wa mtaa wa Malamba Mawili katika kata ya Kwembe Wilayani Ubungo imemalizika baada ya ukamilishaji wa mradi wa maji wenye thamani ya Shilingi Milioni 200 uliokamilika hivi karibuni.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Malamba mawili ndugu, Idd Mgweni ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita Chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha DAWASA kumaliza utekelezaji wa mradi wa maji Kwembe.

"Tunawapongeza Wizara ya Maji kupitia DAWASA kwa kazi hii kubwa walioifanya na nimefarijika kwa sababu kazi hii imekamilika kabla ya muda uliopangwa, na sasa Wananchi wameanza kupata Majisafi na salama," amesema Mwenyekiti Mgweno.

Msimamizi wa mradi, mhandisi Jackson Richard amesema kuwa upatikanaji wa maji katika eneo hilo ni matokeo ya kukamilika kwa mradi wa maji Kwembe ambao umenufaisha zaidi ya wakazi 10,000 wa maeneo ya Kwembe, Malamba mawili pamoja na King'azi ambapo kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya majisafi.

Ameongeza kwamba utekelezaji wa mradi huo, umehusisha ulazaji wa bomba za ukubwa wa inchi 8 kwa umbali wa kilomita 3.5 na kazi ya maboresho bado inaendelea kwa kuwa lengo la Mamlaka ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora zaidi.

"Kazi hii haijaishia hapa, tutaendelea na maboresho kwa kadri yatapohitajika kwani ni jukumu letu Mamlaka kuhakikisha huduma bora kwa wananchi tunaowahudumi" ameongeza Mhandisi Richard.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post