Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MZUMBE NDAKI YA TANGA SASA RASMI! WANANCHI WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUKUZA SEKTA YA ELIMU


Ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya juu kwa Mageuzi ya kiuchumi "HEET Project" leo Agosti 30,2024 Chuo Kikuu Mzumbe kimeendika historia nyingine kwa kusaini mikataba minne ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na kukabidhi kwa Mkandarasi eneo la ujenzi wa kampasi mpya ya Tanga inayoanza kujengwa Wilayani Mkinga katika Kata ya Gombero.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi huo, Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Mhe. Dastan Kitandula ameipongeza Serikali ya Dkt. Samia kwa kufanikisha kupatikana kwa fedha kupitia mradi wa HEET unaolenga kuboresha elimu nchini hasa Vyuo Vikuu ambapo Chuo Kikuu Mzumbe ni miongoni mwa vyuo nufaika.

“Tunaishukuru sana Serikali yetu chini ya uongozi mahiri wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na ndoto yetu ya kuufanya Mkoa wa Tanga kuwa kitovu cha elimu inaanza kutimia kupitia Wilaya ya Mkinga. "Alisema Mhe. Kitandula

Mhe. Kitandula ameahidi kuhakikisha upatikanaji wa huduma zote muhimu zinazohitajika ikiwemo maji, umeme na Barabara ili Mkandarasi aweze kukamilisha kazi kwa wakati. Vilevile ametoa rai kwa wananchi walio karibu na eneo la mradi kutumia fursa zinazotokana na mradi zikiwemo ajira na kutoa ushirikiano unaohitajika.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, amewashukuru wananchi wote wa Tanga hususani Wilaya ya Mkinga kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha kwa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwakaribisha kwa upendo na kuwapa eneo la ujenzi lenye ukubwa wa ekari 300 na kuwaahidi ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi na kwamba chuo kitashughulikia malalamiko yeyote yatakayotokana na utekelezaji wa mradi huo na kuwasisitiza wananchi kuwasilisha changamoto zao kupitia kamati za malalamiko zilizoundwa chini ya ofisi za vijiji na kata yao.

Awali akizungumza, Mratibu wa Mradi wa "HEET" Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Eliza Mwakasangula amesema mradi huo kwa Tanga pekee unagharimu takribani bilioni 12 fedha za kitanzania.

Prof. Mwakasangula amebainisha kwamba mradi huo unategewa kujenga majengo mbalimbali katika Ndaki hiyo ikiwa ni pamoja na jengo la Taaluma, Maktaba, Maabara ya Compyuta, Ukumbi wa Mihadhara, Jengo la Mkahawa, Zahanati na Nyumba za wafanyakazi pamoja na ujenzi wa Tanki la Maji.

Ujenzi wa Kampasi ya Tanga unatekelezwa na kampuni ya wazawa ya Dimetoclasa Real Hope Ltd ambapo Mkurugenzi wa kampuni hiyo bwana Dickson Mwaipopo ameahidi kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ndani ya muda uliopangwa wa miezi kumi na nane.

"Ninaahidi kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili niweze kukamisha kwa wakati na natumaini nitamaliza Ä·abla ya miezi kumi na nane kuisha" alisisitiza Bwana Dickson.

Kwa upande mwingine, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mipango, Fedha na Utawala Prof. Allen Mushi amesema ujenzi huo ni chachu kubwa kwa maendeleo ya watu Mkinga, Tanga na Taifa kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com