NELSON MANDELA YAJA NA TEKNOLOJIA YA UFUGAJI KWA KUTUMIA AKILI MNEMBA



Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu , Sayansi naTeknolojia Professa Ladslaus Mnyone akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mradi wa Tathimini ya Ufanisi wa Teknolojia za Kisasa za Ufugaji unaoratibiwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela leo Agosti 5, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Corridor Spring Arusha.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mradi wa Tathimini ya Ufanisi wa Teknolojia za Kisasa za Ufugaji unaoratibiwa na Taasisi hiyo Agosti 5, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Corridor Spring Arusha.


Mratibu wa Mradi kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Gabriel Shirima akieleza lengo la mradi kwa washiriki na baadhi ya wafugaji Agosti 5, 2024 ukumbi wa mikutano wa Corridor Spring Arusha.


Mtafiti Kiongozi kutoka Chuo Kikuu cha Florida cha Nchini Marekani Dkt. Geoffrey Dahl ( kushoto) na Dkt. Hendrickx Saskia (kulia) wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa mradi wa Tathimini ya Ufanisi wa Teknolojia za Kisasa za ufugaji Agosti 5,2024 katika ukumbi wa mikutano wa Corridor Spring Arusha.


Washiriki wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa Tathimini ya Ufanisi wa Teknolojia za Kisasa za Ufugaji katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Florida cha Nchini Marekani kwa ufadhili wa Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation Agosti 5,2024 jijini Arusha.


Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia Professa Ladslaus Mnyone (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa Tathimini ya Ufanisi wa Teknolojia za Kisasa za Ufugaji unaoratabiwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Florida cha Nchini Marekani kwa ufadhili wa Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation Agosti 5,2024 jijini Arusha.

........ Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imezindua rasmi utekelezaji wa mradi wa Tathimini ya Ufanisi wa Teknolojia za Kisasa za ufugaji kwa kutumia Akili Mnemba (artificial intelligence) lengo ikiwa ni kuwasaidia wafugaji wa ng'ombe wa maziwa na nyama kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo Agosti 5, 2024 mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu , Sayansi naTeknolojia Professa Ladslaus Mnyone ameeleza kuwa, teknolojia hizo zitaleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya mifugo kwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa.

"Kuna changamoto mbalimbali kwa wafugaji wa ng'ombe wa maziwa ikiwemo uzalishaji mdogo na malisho haba, hivyo kupitia mradi huu utarahisisha kwa kutoa taarifa za awali kwa wafugaji kuelewa majira ya uhamalushaji hivyo kuongeza uzalishaji wa maziwa na chakula cha kutosha " anasema Prof. Mnyone.

Aliongeza kuwa, ni budi matokeo ya utafiti na ubunifu mbalimbali zinazofanywa ziwafikie walengwa hususani watumiaji na wananchi kwa ujumla ili waweze kunufaika nazo.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Taasisi Prof Maulilio Kipanyula alieleza kuwa, mradi huo utatekelezwa kwa miaka mitatu ambapo kutaanzishwa Kitovu cha Maarifa kuhusu ufugaji wa mifugo ambacho kitashirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi ya teknolojia hizo za kisasa.

Mtafiti Kiongozi kutoka Chuo Kikuu cha Florida cha nchini Marekani ,Dk. Geoffrey Dahl alisema, mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Bill &Melinda Gates utaleta tija kwa wakulima katika jamii za kimaasai na baadhi ya ranchi ili kutatua changamoto za wafugaji na kupata mifugo bora ikiwemo kupata ndama ambao watatokana na ng'ombe bora wa maziwa.

Naye Mratibu wa Mradi huo, kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) Profesa, Gabriel Shirima alisema mradi huo wa miaka mitatu utawezesha wafugaji kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kufuatilia umbali wa ng'ombe alipotembea kwa siku, ulaji wa nyasi ,kucheua na kutoa taarifa za awali kama mnyama akiwa anaumwa.

Alisema mradi huo, utawezesha ng'ombe wa maziwa kufungwa vifaa vya kisasa aina ya smaXtec bolus itakayosaidia mfugaji kufuatilia kwa karibu tabia za ng'ombe wake kupitia mfumo uliounganishwa na simu ya kiganjani ikiwemo kujua kiwango cha chakula au maji ambacho amekula au kunywa kwa siku.

Lakini pia atatoa maziwa kwa kiasi gani kulingana na uzalishaji huku kifaa cha Ceres tag ambacho ni mfano wa hereni kitatumika kwa kumvalisha sikuoni ng'ombe mmoja katika kundi la ng'ombe wafugwao katika jamii za kimaasai.

Mradi wa Tathimini ya Ufanisi wa za Kisasa za Ufugaji unashirikisha Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Chuo Kikuu cha Florida cha Nchini Marekani MAP Scientific Services (Ceres Tag), SmaXtec (Bolus Monitoring System) kwa ufadhili wa Bill and Melinda Gates Foundation.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post