Na Zena Mohamed,Dodoma
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imefanikiwa kuokoa upotevu wa fedha za serikali kiasi cha TZS: 567,636,151,996.00 katika mshauri 140 yaliyokuwa katika hatua mbalimbali za michakato ya ununuzi wa umma kwa kipindi cha miaka mitatu (2021 – 2024).
Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando amebainisha hayo alipozungumza na waandishi wa Habari katika maonesho ya Kilimo ya Kimataifa (Nane Nane), yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.
“PPAA imeendelea kudhibiti taasisi nunuzi kukiuka taratibu za kisheria hasa katika kufanya tathmini ya zabuni (tender evaluation); katika baadhi ya mashauri ambapo ilifanikiwa kubaini ukiukwaji wa taratibu za kufanya tathimini uliofanywa na taasisi nunuzi ikiwemo kutokuzingatia vigezo vilivyowekwa katika kabrasha la zabuni au kuongeza vigezo vipya ambavyo havikuwepo awali,” alisema Bw. Sando.
Bw. Sando aliongeza kuwa kwa kufanya hivyo, Mamlaka hiyo ilihakikisha kuwa zabuni zinatolewa kwa wazabuni wenye sifa na hivyo kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha na kuepusha upotevu wa fedha za serikali kiasi cha TZS: 567,636,151,996.00 katika michakato ya ununuzi wa umma kwa kipindi cha miaka mitatu.
“PPAA imeweza kushughulikia jumla ya mashauri 140 yaliyotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma kwa kudhibiti utoaji wa tuzo kwa wazabuni ambao walipendekezwa kupata zabuni bila kuwa na sifa stahiki,” aliongeza Bw. Sando.
Aidha, Bw. Sando aliongeza kuwa PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa wazabuni 32 wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika na kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha. Hatua hiyo iliepusha utekelezaji usioridhisha wa miradi ambao ungesababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.
“Serikali ya awamu ya Sita inaamini kuwa usuluhishi wa migogoro hauwezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia. Hivyo, kitendo cha PPAA kuzuia utoaji wa tuzo kwa wazabuni 32 waliokosa sifa kinaweka uzito katika usuluhishi wa migogoro ambayo ni moja kati ya falsafa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Bw. Sando.
Katibu Mtendaji wa PPAA ameongeza kuwa Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Mamlaya ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imejenga moduli mpya ya kuwasilisha Rufaa/Malalamiko kwa njia ya kieletroniki (Complaint & Appeal Management). “Moduli hiyo inarahisisha uwasilishaji wa malalamiko na kutoa fursa kwa wazabuni wengi zaidi kuwasilisha malalamiko yao, ni rafiki na inaokoa muda wa kuwasilisha rufaa,” alisema Bw. Sando.
Aidha, Moduli ya Complaint & Appeal Management imewekwa kwenye Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kieletroniki (NeST), uliojengwa chini ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi ya Umma Na. 3 ya Mwaka 2001 ambapo baada ya Sheria hiyo kufutwa, Mamlaka ya Rufani ilihuishwa chini ya Sheria ya Ununuzi ya Umma Na. 21 ya Mwaka 2004 na kuhuishwa tena kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 baada ya ile Sheria Na. 21 ya Mwaka 2004 nayo kufutwa. Mwaka 2023 Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 nayo ilifutwa na Mamlaka ya Rufani ilihuishwa tena kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya Mwaka 2023.