Na Happiness Shayo - Morogoro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi na Serikali kutunza na kuyalinda maeneo ya hifadhi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae huku akiwaonya Madiwani na Wabunge wenye tabia ya kuanzisha Vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi hasa kipindi cha kuelekea uchaguzi kuacha tabia hiyo.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa CCM Ifakara, Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro leo Agosti 5,2024.
“Inapokaribia kipindi cha uchaguzi hasa Madiwani na Wabunge mtu akiona hayuko vizuri kwenye eneo lake anasogeza watu kuanzisha Kijiji halafu ni haohao wanaokuja kusimama kuwatetea watu walioingia ndani ya hifadhi. Ndugu zangu wanasiasa wenzangu acheni haya” amesisitiza Rais Samia.
Amefafanua kuwa maeneo hayo yanahifadhiwa kwa makusudi maalum kwa faida na maendeleo ya nchi kwa sababu watu wanaongezeka lakini ardhi haiongezeki hivyo ni lazima kuwa na ardhi iliyohifadhiwa kwa matumizi ya baadae
Rais Samia ameielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inahifadhi na kulinda maeneo inayoyasimamia na si kusubiria wananchi wavamie kisha kuwatoa.
“Mpaka wananchi wanahamia wanajenga shule, kituo cha afya bado mnawaangalia baadae wameshatulia ndio mnawaambia watoke wamevamia, hii nayo sio haki” Rais Samia amesema.
Rais Samia yuko Mkoani Morogoro kwa ajili ya ziara ya kikazi ya kuzindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuangalia utekelezaji wake pamoja na kuzungumza na wananchi.