Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango akipewa maelekezo na mtaalamu wa kiwanda cha Mvinyo cha Chinangali II-Chamwino wakati wa Kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho.
NA DOTTO KWILASA, DODOMA
Dodoma ni mji mkuu wa Tanzania na kitovu cha uzalishaji wa zabibu nchini Tanzania .
Umaarufu na upekee wake unatokana na uzalishaji wa zao la zabibu umeishawishi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi mahiri wa Dk. Samia Suluhu Hassan kuanzisha kiwanda cha kuchakata mvinyo Wilayani Chamwino kwenye kijiji cha Chinangali II ambacho kinatazamwa kama fursa inayoweza kubadilisha taswira ya uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa kwa wakazi wa eneo hili.
Kiwanda hicho cha Kusindika Zabibu ambacho kipo chini ya Wizara ya Kilimo kupitia mradi wa Jenga kesho iliyo Bora(BBT)kinagharimu shilingi Bilioni 2.1 za kitanzania na kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchakata Tani 300 kwa mwaka na kuhifadhi lita Milioni 2.2 za mchuzi wa zabibu kwa mwaka.
Kiwanda hicho kitahudumia wakulima takribani 120 kutoka katika maeneo ya Dodoma na karibu na kiwanda huku Serikali ikiweka msukumo zaidi wa kuongeza uzalishaji wa Zabibu kutoka kwenye shamba la zabibu la BBT Chinangali linalomilikiwa na kiwanda hicho.
Wakazi wa eneo hili wanalichukulia zao la Zabibu ya Dodoma sio tu ni chakula, bali pia ni chanzo cha kipato kwa wakulima wengi na fursa za biashara na kwamba kilimo cha Zabibu zimekuwa sehemu ya maisha yao kwa miaka mingi .
Eliasi Joel ambaye ni mkulima wa Zabibu ameeleza kuwa mchango wa Serikali katika kuboresha kilimo cha zabibu umeonekana kupitia kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo na usindikaji wa zabibu.
Anataja faida ya Zabibu kuwa ni chanzo kizuri cha virutubisho, ikiwa ni pamoja na vitamini C, K, na antioksidanti, hivyo kuchangia katika kuboresha afya ya jamii.
Hata hivyo anaeleza changamoto za kilimo hicho kuwa mara nyingi kinakumbwa na mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa teknolojia sahihi, na masoko duni ni vikwazo vinavyokabili wakulima na kueleza kuwa wakulima wanahitaji elimu zaidi kuhusu usimamizi wa mashamba na usindikaji wa mazao ili kuongeza ubora na uzalishaji.
Naye Queen Chalo amesema mbali na kuimarika kwa mfumo mzima wa zao hili,jamii inapaswa kulichukukia kwa uzito huku akiitwisha mzigo Serikali kuona namna ya kutumia zao hilo kama sehemu ya Utalii.
"Wakulima tunategemea zao hili kupaishwa kimataifa,na ili kuimarisha sekta ya zabibu Dodoma, ni muhimu kwa serikali kutilia mkazo kilimo cha mwagiliaji,kuanzisha miradi ya umoja wa wakulima ili kuongeza nguvu na kupunguza gharama ikiwa ni pamoja na kuendeleza soko la ndani na nje, "ameeleza na kuongeza;
Ili kufanikisha haya lazima kuwepo na mpango madhubuti wa kuondokana na changamoto ya upotevu wa maji ardhini ili badala ya kusubiri mvua tutumie umwagiliaji, tunashukuru kuona Serikali tayari imeanzisha mradi wa uchimbaji wa mabwawa katika wilaya za Chamwino na Kongwa,"anaeleza Mkulima huyo wa Zabibu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango anaona umuhimu wa kilimo cha zabibu na kueleza kuwa Serikali inalichukulia zao hilo kuwa ni la kimkakati hivyo ni lazima wakulima watengewe ardhi ya kutosha kuendana na mahitaji ya kiwanda hicho.
Akizungumza Agosti 19 mwaka huu mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye kiwanda hicho Dk.Mpango anaeleza Serikali inalitambua zao la zabibu kuwa ni la kimkakati hivyo kuwataka wakulima wa zabibu kuongeza juhudi zaidi ili kupata mazao mengi na kuboresha maisha yao hali itakayochangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha Dkt. Mpango ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha ardhi inayotengwa kwaajili ya kilimo cha zabibu inalindwa ili usifanyike ujenzi wa makazi katika ardhi hiyo.
"Kasi ya ujenzi wa makazi imekuwa kubwa mkoani Dodoma hivyo ni vema wataalamu wa mipango miji na wapimaji viwanja kuzingatia maeneo ya kilimo cha zabibu kubaki kama yalivyopangwa,nawasihi wananchi wa mkoa wa Dodoma kuongeza jitihada katika kulima zabibu ili kiwanda hiki kiwe na manufaa zaidi, "anasisitiza Dk. Mpango
Anafafanua kuwa Tanzania hutumia takriban shilingi Bilioni 19.5 kila mwaka kuagiza wastani wa lita milioni 10 za mchuzi wa zabibu nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya ndani hivyo uwepo wa kiwanda hicho unatatua changamoto nyingi za usindikaji na uhifadhi wa zabibu pamoja na kuzuia upotevu kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya kuongezea thamani na uhifadhi.
Ameongeza kwamba Viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ikiwemo zabibu kwa ajili ya matumizi yetu ya ndani na kuuza ziada nje ya nchi ni miongoni mwa vipaumbele muhimu katika agenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya 10/30 – yaani kufikia ukuaji wa asilimia 10 katika Sekta ya Kilimo ifikapo 2030.
Makamu wa Rais amesema Serikali imeliingiza zao la zabibu katika orodha ya mazao ya kimkakati ambayo ni ya kipaumbele katika kuendelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi. Amemuagiza Waziri wa Kilimo kuhakikisha upatikanaji wa miche bora kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Halmashauri za wilaya husika, pamoja na kuimarisha huduma za ugani za zao la zabibu.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma kuepukana na uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto na kukata miti ovyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia wajibu wa kutunza vyanzo vya maji na ardhi oevu ili kuunusuru mkoa huo na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbali na kusisitiza umuhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Mkoa wa Dodoma,anasisitiza kwamba Serikali itazidi kutoa msaada na mikakati ya kuimarisha kilimo cha zabibu na kuhakikisha wakulima wanapata mafunzo na rasilimali zinazohitajika ili kufanikisha maendeleo zaidi.
Hata hivyo Dk. Mpango anaeleza kuwa licha ya Serikali kufufua fursa nyingi za kichumi kwa wananchi wa Dodoma, Mkoa huu unaonekana kuwa na Mchango hafifu kwenye pato la taifa na hivyo kuwahimiza Wananchi kuchangamkia fursa ya uwepo wa kiwanda hicho kuanzisha miradi ya kilimo, viwanda biashara na utalii ili kujiongezea kipato.
"Tumieni fursa ya miradi ya kimkakati iliyopo Dodoma kuongea ubunifu kwa kuwekeza kupitia miundombinu ya usafiri wa Anga, reli na Barabara kama fursa za pekee, ukataeni umaskini,tunajua Dodoma ina ardhi yenye rutuba, mbali na Zabibu endelezeni pia kilimo cha tende,mahindi, mpunga na maharage, kilimo kitawakomboa ikiwa mtawekeza kwa tija,Uwekezaji katika kilimo cha biashara na usindikaji wa mazao kwa kuyaongezea thamani, "anasema
Anasema," Lazima muwe wabunifu wa kuchangamkia fursa,Kuanzisha viwanda vidogo na vya kati, hasa vya usindikaji wa mazao, kunaweza kuongeza ajira na kukuza uchumi wa mkoa,kwa unumla Dodoma tuna fursa nyingi na mojawapo kama serikali tumefayya kazi kubwa Sana kutengeneza miundombinu, wananchi wanaoweza wekezeni kwenye maeneo kama hotel , viwanda na madini,"amesema
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo nchini Hussen Bashe amesema
kiwanda hicho ni matokeo ya kilio cha wakulima wa zabibu mkoani Dodoma kukosa sehemu ya kupeleka zao hilo na hivyo kupelekea kupata hasara mara kwa mara.
Ameongeza kwamba kwa sasa hatua ya pili ya ujenzi wa kiwanda hicho ni kuwajengea matenki wakulima wa zabibu ili waweze kuzalisha na kuwa na uwezo wa kuchagua kuuza zabibu kama tunda au kuuza kama mchuzi baada ya kuchakata.
"Kutokana na Mkoa wa Dodoma kuwa na upotevu mkubwa wa maji, tayari Wizara ya Kilimo ina miradi ya umwagiliaji ikiwemo ujenzi wa bwawa la kukusanya maji Wilaya ya Chamwino pamoja na mradi wa hekari 11,000 wa kilimo cha umwagiliaji katika Jimbo la Mtera, " anaeleza
Kiwanda hicho cha Kusindika Zabibu kinachogharimu shilingi bilioni 2.1 kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchakata tani 300 kwa mwaka na kuhifadhi lita million 2.2 za mchuzi wa zabibu kwa mwaka.
Kiwanda hicho kitahudumia wakulima takribani 120 kutoka katika maeneo ya karibu na kiwanda ikiwemo shamba la zabibu la BBT Chinangali.
Waziri Bashe anafafanua kuwa Serikali kupitia wizara ya Kilimo imeimarisha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza vituo vya kununulia mazao ya mvinyo hali itakayosaidia wakulima wa zabibu kuongeza uzalishaji na kuuza kwa bei nzuri inayoendana na soko.
"Tunafanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa zabibu ya Dodoma zinafika kwenye masoko makubwa ya kimataifa,tukifanikiwa kwenye hili tutaongeza kipato cha wakulima na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla"anasema na kuongeza;
Mwanzoni uzalishaji ulikuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji yalivyo lakini kupitia kiwanda hiki uzalishaji utaongezeka kwani kitachakata Lita nyingi zaidi za mchuzi wa zabibu na kutengeneza Mvinyo, "anasisitiza
Sambamba na hilo amesema Serikali itaendelea kuwaunga mkono wazalishaji wadogo wa Zabibu ili kulinda soko la zabibu nchini ikiwa ni pamoja na kutoa msaada mkubwa kwa wazalishaji wa zabibu ili kuboresha uzalishaji na kuhakikisha kwamba mazao yao yanapata soko zuri.
"Ili kupeleka Mvinyo ya Dodoma kimataifa zaidi na kuinua kipato cha mkulima mmoja mmoja tunaanza kutekeleza mipango ya kutoa elimu kuhusu mbinu bora za kilimo, kupanua huduma za ushauri wa kilimo, na kuongeza upatikanaji wa vifaa na mbegu bora ya zabibu, " anaeleza
Bashe amesema wizara yake pia inafanya kazi na wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na uongezaji thamani wa zabibu.
" Lengo letu ni kuhakikisha kwamba wakulima wanapata faida kubwa na kuimarisha sekta ya kilimo cha zabibu kwa ujumla."anasema
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameeleza kuwa uwekezaji huo ni muhimu kwa kuwa utachagiza maendeleo ya kiuchumi na ajira katika mkoa .
"Tunashukuru kwa uwekezaji huu mkubwa na wa kimkakati tunaahidi kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji, tunatarajia kuona matokeo chanya yatakayotokana na juhudi hizi."amesema
Amesema kiwanda hicho cha mvinyo kinaweza kuwa kivutio cha utalii ambapo Wageni wataweza kutembelea kiwanda, kujifunza kuhusu mchakato wa uzalishaji wa mvinyo, na kufurahia ladha tofauti za mvinyo, hivyo kukuza sekta ya utalii katika mkoa wa Dodoma.
"Serikali itafaidika kupitia kodi kutoka kwa kiwanda, ambazo zinaweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo,Kuwepo kwa kiwanda hiki kutasaidia kuongeza kipato cha serikali na kuimarisha huduma za kijamii, " ameeleza
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la chamwino na Waziri wa Ardhi Deo Ndejembi amesema,"Katika wilaya yetu hatuna tunachoidai Serikali kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia ,kupitia kiwanda hiki kitasaidia kuimarisha uchumi kwa wakazi wa Dodoma na kuchangia maendeleo ya jamii, "ameeleza
Ndejembi anaeleza kuwa Kiwanda cha kusindika zabibu kitatoa nafasi za ajira kwa wananchi na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira na kuboresha maisha ya watu katika jamii kwa kuwa WQatu wengi wataweza kupata kazi katika hatua mbalimbali za uzalishaji, usindikaji, na usambazaji.
"Kiwanda hiki kitachochea uchumi ,Wakulima wa zabibu wataweza kuuza mazao yao kwenye kiwanda na kuwa na soko la uhakika ikiwa ni pamoja na kuleta teknolojia mpya na ujuzi katika jamii watendaji wa kiwanda wataweza kuwafundisha wakulima na wafanyakazi wengine jinsi ya kutumia teknolojia za kisasa katika kilimo na usindikaji, "amesema