Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imesema imejidhatiti kuendelea kufanyia maboresho sheria za ulinzi wa Watoto ili ziweze kuendana na wakati huu wa sasa kwa maslahi mapana ya kuwalinda Watoto.
Hayo yamesemwa leo Agosti 30, 2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), alipokuwa akichangia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Ulinzi wa Mtoto wa Mwaka 2024.
“Sisi kama Serikali ni wajibu wetu kuhakikisha tunaleta Bungeni sheria za Watoto ili zifanyiwe maboresho” Mhe. Chana amesisitiza.
Kuhusu hoja ya namna ya kudhibiti mitandao ya kijamii na uharibifu wa mitandao hususan kwa Watoto, Mhe. Chana ameishukuru Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia kwa kuendelea kudhibiti baadhi link zenye maudhui potofu kwa ajili ya kuwalinda Watoto.
Aidha, amesema pamoja na mambo mengine Serikali imeendelea kuboresha muhimili wa mahakama zikiwemo mahakama za watoto na kupunguza mlundikano wa kesi, kuboresha majengo ya mahakama ambapo kuna mahakama katika wilaya takribani 137 nchini ambako kwenye mahakama zote kuna mahakama za Watoto.
Pia, amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba maamuzi ya kesi za Watoto yanatoka haraka katika mahakama kwa sababu serikali inafahamu watoto wana haki ya elimu huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuteua Majaji na Mahakimu ambao wanaosimamia kesi hizo za Watoto.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chana amesema Serikali imefunga video conference inayowezesha kesi kuendeshwa wakati watuhumiwa/wahalifu wakiwa bado magerezani na pia kwa kuona umuhimu wa elimu kwa Watoto Serikali imejipanga kufanya maboresho kwa kutumia e-learning wakati watoto wakiwa katika vifungo vyao ili kuwepo na haki ya wao kupata elimu.