SERIKALI YAJIZATITI KUNUSURU THELUJI INAYOTOWEKA KATIKA MLIMA KILIMANJARO



Na Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa misitu imezindua kampeni ya kupanda miti zaidi ya Bilioni moja katika mikoa ya kaskazini ili kunusuru barafu ya mlima Kilimanjaro. Kampeni hii ya upandaji miti inakwenda sambamba na utekelezaji wa mikakati ya kupanda zaidi ya miti milioni 8 kwa mwaka katika Mkoa wa Kilimanjaro, utoaji elimu kwa umma kuhusu upandaji miti, na uhifadhi wa mazingira kupitia vipindi vya redio, televisheni, matamasha na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Naibu Waziri wa maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mhe. Prof. Patrick Alois Ndakidemi Bungeni Mjini Dodoma aliyetaka kujua Serikali imechukua hatua gani za muda mfupi, wakati na muda mrefu kunusuru theluji inayotoweka katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Aidha, Mhe. Kitandula alisema kuwa sababu kubwa ya kupungua kwa theluji katika Mlima Kilimanjaro ni ongezeko la joto duniani kutokana na mabadiliko ya Tabia nchi yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu hususan ukataji wa miti, kilimo, uchomaji moto katika maeneo yanayozunguka mlima, uwepo wa mvua chache na vipindi virefu vya ukame, na upepo mkavu kutoka bahari ya Hindi.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa kwa mikakati ya muda wa kati Serikali inajielekeza katika kuhimiza matumizi bora ya ardhi na kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na kutekeleza mipango ya kudhibiti na kupambana na uchomaji moto mlimani.

Aidha, kwa upande wa mikakati ya muda mrefu, Mhe. Kitandula alilieleza bunge kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na mashirika ya kikanda na kimataifa kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na kuboresha teknolojia za kilimo, kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji, kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kurejesha mifumo ikolojia kwenye mlima na maeneo yanayozunguka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post