TANESCO YAPONGEZWA KWA UTENDAJI MZURI



Na mwandishi wetu

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepongezwa kwa utendaji mzuri katika Utekelezaji wa Miradi ya uzalishaji na Usambazaji Umeme nchini pamoja na suala zima la Utoaji Huduma kwa Wadau.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 21 August, 2024 na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa mara baada ya kutembelea Banda la TANESCO katika Mkutano wa 9 wa Wahandisi Wanawake 2024.

Bashungwa ambaye ndiye mgeni rasmi katika maonesho hayo, ameelezea kufurahishwa kwake na hatua nzuri zilizofikiwa na TANESCO katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Umeme nchini pamoja na suala zima la Uboreshaji wa Utoaji Huduma kwa Watumiaji wa Umeme.

Ameitaka TANESCO kuendeleza kasi hiyo ili kuzidi kuboresha huduma za utoaji umeme nchini.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, Watumishi walioshiriki Maonesho hayo wamepokea pongezi hizo na kuahidi kuzidisha kasi ya utendaji na utoaji wa Huduma bora kwa Wadau.

Mkutano huo wa Wahandisi Wanawake unakwenda pamoja na Maonesho yanayoshirikisha Taasisi Mbalimbali hapa nchini.

TANESCO inawakaribisha wadau wote wanaotembelea Maonesho hayo kutembelea Banda la TANESCO ili wapate kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali na pia kupata elimu kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na TANESCO ikiwemo maboresho ya Mita za Luku.

Mkutano huo utafungwa rasmi tarehe 22 Agosti, 2024.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post