Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akichangia mada ya Amani na Utulivu: kuhakikisha Heshima ya Binadamu na Usalama wa Binadamu kwenye sehemu ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.
Waziri Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Yoko Kamikawa akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.
Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akifatilia ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo
Washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa Mkutano huo
*********************
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo na changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo. Pia imemewahimiza wadau wote wa maendeleo kutoka nchini Japan kuendelea kufanya biashara na kuwekeza zaidi barani Afrika ili kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya binadamu katika bara hilo ikiwa ni katika juhudi za kuendeleza amani na utulivu kikanda na kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi alipochangia mada ya Amani na Utulivu: kuhakikisha Heshima ya Binadamu na Usalama wa Binadamu kwenye sehemu ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika nchini Japan tarehe 24-25 Agosti 2024.
Ameipongeza Japan kwa kuwa mstari wa mbele kushiriki katika jitihada za kimataifa na kuwaomba washirika wengine wa kimataifa kuiga mfano huo na kuongeza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa ushiriki sawa na ujumuishaji wa wanawake na wanaume, wasichana na wavulana katika kuhakikisha amani na usalama vinatamalaki.
Amesema kutokana na umuhimu huo Tanzania iko katika hatua za mwisho za kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji (NAP) kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka 2000.
Amesema siku zote Tanzania imekuwa na mchango muhimu katika harakati za upatanishi, mazungumzo ya amani na njia nyingine za kidiplomasia katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa ndani na nje ya mipaka yake na ndio maana imefanikiwa kuondoa mizizi ya vita vya kikabila na migogoro kwa kuunganisha makabila takriban 126 na kutumia lugha moja ya Kiswahili kama lugha ya Taifa.
Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo Tanzania imeendelea na utamaduni wa kuwapatia hifadhi mamia ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka nchi jirani na zaidi na kwa sasa Tanzania inahifadhi wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi wapatao 237,997 huku wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.
Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe.Yoko Kamikawa umehudhuriwa na Mawaziri, washirika wa TICAD, wawakilishi na waandaaji wenza -Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Benki ya Dunia, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na mashirika ya Kimataifa na kikanda, sekta binafsi na Kiraia kutoka Japan na Afrika.
Social Plugin